Mfuasi sugu wa Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga, Nuru Okanga amesema yuko tayari kujiunga na shule ya bweni baada ya kufanya mitihani yake ya KCPE na kufaulu.
Katika mahojiano na Mpasho siku ya Ijumaa, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 32 alifichua kwamba anatamani sana kujiunga na Shule ya kitaifa ya Lenana au Alliance kwa masomo yake ya shule ya upili.
Okanga hata hivyo alisema kuwa mkuu wa shule ambayo atajiunga nayo hatimaye anafaa kuwa tayari kumruhusu kwenda nyumbani na kutembelea familia yake kila wikendi kwa kuwa ana mke na familia ndogo.
"Mimi nafikiria niende Lenana High school, ama Alliance, hizo shule mbili," Okanga alisema.
Mtahiniwa huyo wa KCPE 2023 aliongeza, “Mimi niko tayari lakini yule mwalimu mkuu wa Alliance ama Lenana School atakuwa anahakikisha kila Ijumaa jioni amenipea nafasi niende nyumbani na kuona familia, Jumatatu asubuhi niripoti shuleni.”
Katika mahojiano hayo, mfuasi huyo sugu wa chama cha ODM alielezea kusikitishwa kwake na jinsi Wakenya na vyombo vya habari wanavyofuatilia sana kujua ni alama ngapi alizopata.
Ingawa alikataa katakata kuthibitisha kile alichokipata, alisema ameridhishwa na alama zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidaiwa kuwa ni zake.
“Nilienda nikafanya mtihani kabisa na nikapost. Kila mahali wakajua Okanga amekalia mtihani. Na nilijua siku kama ya leo ama ya jana, kuna vitu zinakuja. Nilikuwa natarajia matokeo na kutrend.. Sasa watu hata wamemuacha namba moja Kenya mzima. Wameacha ata mtihani wenyewe, ata saa hii ukiuliza mtoto ni nani waziri wa elimu hajui. Anajua tu Okanga. Mimi naambia watu wa media, nilifanya mtihani wangu nikaweka hadharani. Kwa hivyo, alama mliweka nimeridhika nayo. Siwezi punguza na siwezi kuongea," Nuru Okanga alisema kwenye mahojiano ya siku ya Ijumaa.
Okanga pia alifichua kuwa timu ya Muungano wa Azimio inayoongozwa na kinara wake Raila Odinga tayari imempongeza kwa kutowaangusha.
Mwanasiasa huyo alifanya mtihani wa KCPE 2023 katika Shule ya Msingi ya Mumias Muslim iliyoko kaunti ya Kakamega na ni miongoni mwa watahiniwa zaidi ya milioni moja waliopokea matokeo yao Alhamisi.
Hapo awali, shabiki huyo sugu wa Raila Odinga mwenye umri wa miaka 32 alifichua kwamba aliamua kurejea shuleni na kukalia mtihani wake wa KCPE kama mtahiniwa wa kibinafsi ili apate vyeti vya kumruhusu kuwania kiti cha MCA wadi ya Kholera, eneo la Matungu katika uchaguzi mkuu wa 2027.