Mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa kosa la kuendesha studio ya filamu na kutengeneza filamu bila leseni halali.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Malindi, Olga Onalo pia alimhukumu kifungo kingine cha miezi sita jela kwa kuwaonyesha wananchi filamu hizo kupitia kituo cha Times TV bila kuwa na leseni ya uendeshaji.
Hukumu hizo zitaendeshwa kwa wakati mmoja lakini Mackenzie ana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 14. Haya yanajiri baada ya Afisa wa uchunguzi anayeshughulikia kesi hiyo kupendekeza kwamba Mackenzie anyimwe chaguo la faini kwa hukumu hiyo.
“Kuhusiana na mashitaka mawili, ninamhukumu mshtakiwa kifungo cha miezi kumi na miwili jela, shtaka la tatu, maelezo ya mshtakiwa kutojua hitaji la leseni kutoka kwa Bodi ya Uainishaji wa Filamu ya Kenya (KFCB) baada ya kupata leseni ya utangazaji yanakubaliwa ingawa hakubaliki kabisa kwani hakuna utetezi kwa kutojua sheria kwa hivyo hiyo, ninamhukumu mshtakiwa kifungo cha miezi sita jela,” alisema Onalo.
Makosa yanayomkabili Mackenzie yanavutia kifungo cha jela kisichozidi mwaka mmoja na faini mbadala isiyozidi shilingi laki moja.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa kortini ilitokana na agizo la mahakama lililoelekeza afisi ya uangalizi wa sheria kutunga ripoti ya kuongoza kuhukumiwa kwa Mackenzie katika kesi ya mwaka wa 2019 inayohusu kuendesha studio ya kurekodi na televisheni bila leseni halali kutoka KFCB.
Ripoti ya idara ya uchunguzi Mombasa ilieleza kuwa katika rekodi za awali za uhalifu, Mackenzie alipatikana na hatia na kutozwa faini kwa kosa sawa na hilo mwaka 2017.