Waziri wa elimu wa Machogu ametangaza hatima ya wanafunzi Zaidi ya elifu mbili ambao kwa njia moja au nyingine walikosa kufanya mitihani yao ya darasa la nane, KCPE mwaka 2023.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne, KCSE kutoka shule ya upili ya wasichana ya Moi mjini Eldoret, waziri Machogu alisema kwamba awali walikuwa wamepanga wanafunzi hao kukalia mitihani hiyo kabla ya Januari lakini haingewezekana.
Alisema kwamba huku watahiniwa wenzao ambao walipata mitihani wakijiandaa kujiunga na kidato cha kwanza kuanzia wiki kesho, hao pia watakubaliwa kujiunga shule za sekondari licha ya kutofanya mitihani ya KCPE.
“Ningependa kuweka wazi pia kuwa Zaidi ya wanafunzi 2000 ambao walikosa kufanya mitihani yao ya KCPE katika kundi la mwisho la 2023 wataruhusiwa kujiunga na shule za upili kuanzia Jumatatu Januari 15 lakini watahitajika kukalia mitihani hiyo ya kufuzu baadae. Pia tutahakikisha wanakalia mitihani ya kibinafsi ya kufuzu kabla ya kujiunga kidato cha 3 ili kuhakikisha watasajiliwa kufanya mitihani ya kidato cha 4 KCSE,” Machogu alibainisha.
Itakumbukwa kwamba kikundi cha watahiniwa wa 2023 katika mitihani ya KCPE ndicho kikundi cha mwisho kabisa kufanya mitihani hiyo ambayo inahitimisha mtaala wa 8-4-4 ambao umekuwa kwenye mtumizi kwa miaka 38.
Hii ina maana kwamba mwanafunzi ambaye alifeli kufanya KCPE hatoweza kurudi tena katika darasa la nane kwani mtaala wa CBC ndio utaingia gredi ya 8 mwaka huu, na kama mwanafunzi huyo atataka kujiunga na mtaala huo mpya, basi itamlazimu kurudi hadi gredi ya 4.