Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) inaendelea na uchunguzi kuhusu kisa cha mlipuko hatari wa gesi uliotokea katika mtaa wa Embakasi, Nairobi mnamo Februari 1, 2024, na kuua watu watatu papo hapo na kuwaacha wengine wengi na majeraha tofauti.
Katika ripoti ya Jumanne asubuhi, Februari 6, wapelelezi walifichua kuwa kufikia sasa, watu wanne wamekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi kuhusiana na tukio hilo la kusikitisha.
Mfanyibiashara anayeaminika kuwa mmiliki wa eneo hilo haramu la kujaza gesi, Derrick Kimathi ni miongoni mwa wale ambao wamekamatwa. Maafisa watatu wa NEMA pia wako kizuizini.
Idara ya DCI inaendelea na msako wa washukiwa wengine watano waliohusishwa na tukio hilo la mapema Februari ambao wanaripotiwa kuwa mafichoni
Kufikia sasa, waathiriwa sita wa mlipuko huo mbaya wa gesi wamefariki huku watu wengine wapatao mia tatu wakiripotiwa kujeruhiwa kwa viwango tofauti vya moto.
Baadhi ya waathiriwa walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku wengine wakiwa bado wamelazwa katika hospitali mbalimbali wakiwa katika hali tofauti.