Bunge la Madagaska hivi majuzi limepitisha sheria mpya inayoidhinisha kunyofolewa kwa korodani kupitia upasuaji kwa watuhumiwa wa ubakaji wa watoto watakaopatikana na hatia hiyo.
Hatua hii inaakisi sheria kama hiyo iliyotungwa hivi majuzi nchini Kazakhstan, ambapo wakosaji wabaya zaidi wa kufanya ngono na watoto watafanyiwa upasuaji wa kuondolewa sehemu za siri.
Mnamo Februari 2, Bunge la Kitaifa la Madagaska liliidhinisha sheria hiyo, inayoruhusu kuondolewa kwa korodani za watu waliopatikana na hatia ya kubaka watoto.
Chini ya sheria ya awali, wahalifu wa uhalifu huo walikabiliwa na hukumu ya kuanzia miaka mitano hadi 20 ya kazi ya kulazimishwa.
Hata hivyo, sheria hiyo mpya inabainisha kuwa wale watakaopatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa chini ya umri wa miaka kumi watafanyiwa upasuaji wa kuondolewa korodani zao na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, kwa mujibu wa Mail Online.
Katika hali ambapo mwathirika ana umri wa kati ya miaka kumi na 13, wahalifu badala yake wataondolewa korodani kwa kemikali na kutumikia miaka 15 hadi 20 ya kazi ya kulazimishwa.
Watoto wadogo watakaopatikana na hatia ya uhalifu kama huo hawataruhusiwa kunyofolewa.
Waziri wa Sheria Landy Randriamanantenasoa ameelezea kuunga mkono mswada wa kunyofolewa korodani kwa wabakaji wa watoto wachanga.
Le Quotidien, gazeti la lugha ya Kifaransa, lilimnukuu Bi Randriamanantenasoa akisema, "Jamii lazima ijue walifanya nini na wao ni nani."
Mswada huo, uliopendekezwa na Rais wa Madagascar Andry Rajoelina mwezi uliopita, ulikuwa msingi wa ahadi zake za uchaguzi wa marudio mwaka jana.