Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka anasema muungano wa Azimio la Umoja One Kenya bado utasalia imara bila ya uwepo wa kiongozi wao Raila Odinga katika siasa za humu nchini.
Musyoka anayasema haya wakati ambapo Odinga yumo mbioni kujikita katika kuwania kuwa mwenyekiti wa tume ya muungano wa Afrika, AU – hivyo kuacha hatma yake ya siasa za ndani katika hali tete.
Kalonzo hata hivyo alisisitiza kwamba hii si mara ya kwanza kwa Raila kupata nafasi ya kufanyia kazi bara zima la Afrika.
Odinga wiki jana alitangaza wazi azma yake ya kuwania kuwa mwenyekiti wa tume ya AU, nafasi ambayo inashikiliwa na Moussa Faki kutoka Chad ambaye hatamu yake ya uongozi wa miaka 10 unakamilika Janauri mwaka 2025.
Tangu wakati huo, Odinga amepata uungwaji mkono maradufu kutoka kwa baadhi ya viongozi wakuu barani akiwemo rais wa zamani wa Nigeria Olesegun Obasanjo.
Kalonzo alikuwa akizungumza wakati wa kuwahutubia wananchi katika soko la Kenyatta Jumapili alasiri.
“Baba [Raila Odinga] amekuwa mkubwa kushinda mambo haya, tumpigieni makofi. Na kwa hivyo kazi iliyoko hapa ni kuwahakikishieni nyinyi kwamba Azimio la Umoja One Kenya tuko imara. Siku ya pili baada ya Baba kusema anataka kazi hii, tulikutana na wenzangu, na tukakubaliana ni lazima Azimio la Umoja tukae ngumu na kutetea haki za Wakenya” Kalonzo alisema kwa sehemu.
Katika msafara huo, Kalonzo alikuwa ameandamana na katibu wa chama cha ODM ambaye pia ni seneta wa kaunti ya Nairobi, Wakili Edwin Sifuna.