Spika wa bunge la Kenya ameiagiza wizara ya elimu kuchunguza madai kuwa chuo kikuu kimoja nchini humo kimekuwa kikiwalazimisha wanafunzi wa kiislamu kuhudhuria ibada za dini ya kikristo.
Chuo Kikuu cha Daystar, taasisi binafsi ya Kikristo nje kidogo ya mji mkuu, Nairobi, pia inashutumiwa kwa kuwanyima alama wanafunzi wanaokataa kuhudhuria ibada za kanisa.
Chuo kikuu kimekanusha hili na kusema hakizuii alama za wale ambao hawahudhurii kanisa hilo, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
Madai hayo yalitolewa bungeni na mbunge wa Kenya Mohammed Ali, ambaye alisema sera hiyo inakiuka haki ya kikatiba ya uhuru wa kidini.
Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alitoa majibu ya chuo hicho akisema: "Chuo kikuu kilisema kuwa wanafunzi wote wanadahiliwa wakiwa na ufahamu kamili kwamba chuo kikuu ni taasisi ya Kikristo yenye falsafa, maadili yake ya msingi". “Baada ya kudahiliwa, wanafunzi hutia saini kanuni za maadili ambazo kwazo wanakubali kufuata maadili ya Kikristo ya chuo kikuu na kujitolea kushiriki katika taaluma za kiroho za chuo kikuu,” aliongeza, akitoa mfano wa chuo kikuu.
Chuo kikuu pia kilimweleza Bw Machogu kwamba wanafunzi wanahitajika kuhudhuria angalau 75% ya huduma za kanisa kila muhula.
Wizara ya elimu pia itachunguza ripoti za Bw Ali kwamba taasisi hiyo inaendeleza desturi za LGBTQ kwa kujumuisha masuala ya LGBTQ katika mtaala wake.