Polisi wote kote nchini ambao wamehudumu kwa zaidi ya miaka mitatu katika kituo kimoja watahamishwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki ameamuru kuhamishwa mara moja kwa maafisa wa polisi ambao wamekuwa katika eneo moja kwa zaidi ya miaka mitatu. Kindiki aliangazia kuwa baadhi ya maafisa hao wamezembea kutokana na kukaa kwa muda mrefu katika eneo moja.
“Tumezungumza kuhusu suala hili la sera ya uhamisho ya miaka 3 kwa muda mrefu sana na nilitaka kuwasiliana kwamba maofisa kutoka vikosi vyote waliotumikia kituo kimoja kwa miaka mitatu na zaidi watahamishwa kuanzia leo (Ijumaa, Machi 8, 2024) ," Kindiki alisema.
Waziri huyo pia alidokeza kwamba maafisa hao wameendeleza maslahi ya kibinafsi yanayohusiana na vituo walivyopangiwa, jambo ambalo anasema linazuia ufanisi wao katika kutimiza majukumu yao kama mamlaka ya kutekeleza sheria.
Zaidi ya hayo, Kindiki alisema kuwa baadhi ya maafisa hao hufumbia macho vitendo vya uhalifu, kujihusisha na kuwakinga wahalifu ili wapewe rushwa.
"Wana masilahi ya ndani na wamejiingiza kwenye biashara, wengine wameoa hata kwenye jamii na ndio wanaingia kwenye mashirikiano machafu na baadhi ya watu wanaoharibu nchi, ndio wanaopanga ada za ulinzi," Waziri Kindiki alisema.
Kulingana na sera ya serikali afisa wa polisi hafai kuhudumu katika kituo kimoja cha polisi kwa zaidi ya miaka mitatu. Sera hii inalenga kuhumisha utendakazi wa maafisa wote wa usalama.