Watu wanne walifariki papo hapo huku wengine kadhaa wakipata majeraha wakati gari walilokuwa wakisafiria lilipohusika katika ajali katika eneo la Koroma kaunti ya Kirinyaga Jumamosi usiku.
Polisi walisema ajali hiyo ilitokea kando ya barabara ya Ngaru - Gatuto.
Dereva wa gari la abiria 14 (PSV), almaarufu Matatu, alikuwa akiendesha kutoka Kerugoya kuelekea Kagio kupitia barabara ya Ngaru - Gatuto alipopoteza udhibiti wa gari hilo.
Dereva alikuwa akijaribu kupiga kona kali wakati gari lilibingiria mara kadhaa.
“Kutokana na athari hiyo, abiria wanne walifariki dunia papo hapo huku wengine wakipata majeraha na kukimbizwa katika Hospitali ya Kerogoya ambako waliachwa wakiendelea na matibabu,” polisi walisema.
Miili ya waliofariki ilihamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kerugoya ikisubiri uchunguzi wa maiti.
Gari hilo lililoharibika vibaya lilivutwa hadi Kituo cha Polisi cha Kerugoya ambako lilizuiliwa likisubiri kufanyiwa ukaguzi.