Mwanawe rais wa zamani wa Guinea-Bissau amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela na mahakama ya Marekani kwa kuongoza mtandao wa kimataifa wa ulanguzi wa dawa za kulevya.
Malam Bacai Sanha Jr, 52, alipanga kutumia mapato hayo kufadhili azma yake ya kuwa rais wa Guinea-Bissau kupitia mapinduzi, mamlaka zilisema.
Yeye ni mtoto wa Malam Bacai Sanha, ambaye aliongoza nchi hiyo ya Afrika Magharibi kutoka 2009 hadi kifo chake mwaka 2012.
Sanha Jr amehusishwa na mapinduzi yaliyofeli mnamo Februari 2022.
Alirejeshwa Marekani mnamo Agosti 2022, kufuatia kukamatwa kwake nchini Tanzania wiki chache zilizopita.
Kesi yake ilianza kusikilizwa muda mfupi baadaye na Septemba mwaka jana, alikiri kosa la kula njama ya kuingiza dawa za kulevya kinyume cha sheria.
"Malam Bacai Sanha Jr hakuwa mlanguzi wa kimataifa wa dawa za kulevya," afisa wa FBI Douglas Williams alisema Jumanne.
"Yeye ni mtoto wa rais wa zamani wa Guinea-Bissau na alikuwa akisafirisha dawa za kulevya kwa sababu maalum - kufadhili mapinduzi ambayo hatimaye yangemwezesha kuwa urais wa nchi yake ya asili ambapo alipanga kuanzisha utawala wa madawa ya kulevya."
Mamlaka ya Marekani inasema Sanha Jr anaweza kufukuzwa nchini kufuatia kufungwa kwake kwani yeye si raia wa Marekani.
Sanha Jr mwenye umri wa miaka 52, anayejulikana kwa jina la "Bacaizinho" nchini Guinea-Bissau, ameshikilia majukumu kadhaa serikalini, ikiwa ni pamoja na kuwa mshauri wa kiuchumi wa babake.