Aliyekuwa msemaji wa baraza lililokuwa liiendesha kampenzi za uchaguzi wa urais kwa mgombea wa Azimio Raila Odinga, Makau Mutua amesuta vyombo vya habari vinavyoendesha magazeti na majarida kwa kukwepa kuchapisha habari zozote kumhusu Brian Chira.
Mutua kupitia ukurasa wake wa X, alisema kwamba magazeti ya nchini Kenya yalifanya makusudi kwa kukwepa kuchapisha habari zozote kuhusu kifo na mazishi ya tiktoker huyo aliyezikwa Jumanne.
Msomi huyo ambaye ni mhadhiri katika chuo kimoja Marekani alisema kwamba magazeti yalipotoka katika wajibu wao wa kutaarifu, walipoamua kutochapisha habari zozote kuhusu mazishi ya kijana huyo, licha ya kuwa gumzo katika mitandao ya kijamii kwa jinsi mazishi yake yalitikisa.
“INASIKITISHA magazeti ya Kenya yameepuka KWA MAKUSUDI kutoa habari za kweli, za kina, na za kufikiria kuhusu mazishi - na matukio - ya BRIAN CHIRA,” Profesa Makau Mutua alisema.
Msomi huyo alisema kwamba kwa jinsi watu wengi walifurika katka mazishi ya Chira, kijana huyo alikuwa ni kama sumaku kwa vijana na inasikitisha kuona jinsi magazeti yalipuuzilia mbali kulizungumzia tukio hilo.
“Kijana huyo alikuwa ni kifurushi cha kuvutia kwa vijana wa Kenya pamoja na ahadi yake kuu. Alitufundisha masomo mengi. AIBU!” Mutua aliongeza.
Chira alifariki takribani wiki mbili zilizopita katika ajali ya barabarani kwa kugongwa na gari.
Tangu kifo chake, jamuiya ya TikTok nchini Kenya imekuwa ikiendesha mipango yote ya mazishi yake mpaka siku ya mazishi, asilimia kubwa ya waombolezaji ilijumuisha tiktokers kutoka kila kona ya nchi.