Gavana wa jimbo la Meru, Kawira Mwangaza amewafurahisha wengi kwa ujumbe mtamu wenye wingi wa makopakopa aliomtungia mumewe Murega Baichu kumsherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook, gavana Mwangaza alichapisha rundo la picha zinazoonyesha nyakati nzuri za munganiko wao na kumsifia kwa maneno mengi mazuri yanayodondokwa utamu.
Alimtaja kama mwanamume mtanashati Zaidi ambaye amewahi kutana naye na kusema Baichu ni mtu anayependelewa Zaidi kote Afrika.
Pia gavana huyo alimtaja Baichu kama mtu mwenye taaluma ya kuwa mume na kuapa kuendelea kumpenda.
“Heri njema ya siku ya kuzaliwa M'verified wangu, M’permanent wangu, mume mtaalamu, Kamanda wa Ameru Airwaves, Mshauri wangu Mkuu Mtendaji, Mwanaume Mtanashati na Anayependelewa zaidi Afrika, mpenzi mwenyewe, mshirika wangu wa chumbani, na mume wa kwanza wa kaunti mwenyewe,” Mwangaza aliandika kwa njia ya kishairi.
Baichu alijibu kwa ujumbe rahisi lakini mzito, akisema, "mume mtaalamu ana furaha."
Hii si mara ya kwanza kwa Gavana Mwangaza kusherehekea hadharani siku ya kuzaliwa ya mumewe.
Mwaka jana, aliandika barua kama hiyo ya upendo, akionyesha upendo wake kwa maneno ya kupendeza.
Hata hivyo, maonyesho ya hadharani ya Gavana Mwangaza ya mapenzi kwa mumewe yamekuwa bila utata. Mwishoni mwa mwaka jana, alizua tafrani kwa kuitaja barabara iliyorekebishwa jina la mume wake, na kusababisha shutuma za upendeleo na hata jaribio la kufunguliwa mashtaka, ambapo alinusurika kutimuliwa ofisini.