Serikali ya taifa jirani la Uganda imearifiwa kutangaza mpango wa kutolewa kwa korodani kwa mbwa wote wa kiume wanaotangatanga nchini humo kutokana na kile kilichotajwa kuwa ongezeko la visa vya mbwa kuwashambulia watu kwa kuwang’ata.
Tangazo hilo la lililochapishwa kwenye toleo la Daily Monitor lilisema mamlaka ya jiji la Kampala, KCCA inapanga kung'oa korodani za mbwa wapatao 8,000 kama njia moja ya kuzuia kuenezwa kwa ugonjwa wa ‘rabies’ unaotokana na kuumwa na mbwa.
Kaimu Ofisa mifugo wa wilaya hiyo, Dk Herbert Kasiita, alisema takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuna mbwa 6,000 waliozurura, huku mbwa wengine 2,000 wakiwa na wamiliki ambao hawawatunzi.
Dk Kasiita alifafanua mbwa aliyepotea kama mbwa anayemilikiwa ambaye amepoteza makazi yake. Alisema mbwa wa aina hiyo ni wengi sokoni, kwenye machinjio na sehemu zinazochomwa nyama.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa taifa hilo kutangaza mpango huu kabambe kama njia moja ya kuzuia visa vya watu kuambukizwa ugonjwa kwa kung’atwa na mbwa.
Septemba 2022, Wizara ya Kilimo, Sekta ya Wanyama na Uvuvi ilitangaza kuendesha zoezi la kuwang’oa korodani mbwa na paka waliozurura kama mojawapo ya afua za kupambana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa nchini humo.
Hatua hiyo ilitangazwa kama moja ya shughuli za kuadhimisha Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani iliyopangwa kufanyika Septemba 28, 2022.