logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mafuriko yasababisha uharibifu mkubwa Kenya

Katika kilipu ya video, wakazi wanaonekana wakiwa wamenaswa kwenye paa la nyumba yao.

image
na Davis Ojiambo

Habari25 April 2024 - 05:27

Muhtasari


  • • Jumatano asubuhi, Shirika la Reli la Kenya lilisema mafuriko hayo yameathiri njia za reli, na hivyo kufanya kuwa vigumu kwa treni kufanya kazi.

Barabara zimegeuka kuwa mito katika mji mkuu wa Kenya Nairobi, huku afisa wa ngazi ya juu akisema mafuriko "yameongezeka na kufikia viwango vya kutisha".

Mvua kubwa imenyesha nchini Kenya katika siku za hivi karibuni, na kusababisha uharibifu mkubwa.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa takriban watu 32 wamepoteza maisha na zaidi ya 40,000 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mvua na mafuriko.

Edwin Sifuna, ambaye ni Seneta wa Kaunti ya Nairobi, alizua taharuki kwenye mtandao wa kijamii wa X huku akichapisha picha zinazoonyesha mtaa mzima uliosombwa na mafuriko.

Katika kilipu hiyo ya video, wakazi wanaonekana wakiwa wamenaswa kwenye paa la nyumba yao.

Mamia ya wengine jijini Nairobi na maeneo ya karibu pia walikumbwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha.

"Tunahitaji huduma zote za dharura za kitaifa kuhamasishwa ili kuokoa maisha," Bw Sifuna alisema.

Jumatano asubuhi, Shirika la Reli la Kenya lilisema mafuriko hayo yameathiri njia za reli, na hivyo kufanya kuwa vigumu kwa treni kufanya kazi.

Kampuni hiyo ilisema hofu ya usalama iliilazimisha kusitisha huduma zake.

Barabara kuu, zikiwemo ile ya Mombasa na Thika, zilijaa maji ya mafuriko, na kusababisha msongamano wa magari nyakati za asubuhi.

Barabara yenye shughuli nyingi ya Namanga, inayoelekea mpaka wa Tanzania, ilifurika baada ya Mto Athi ulio karibu kuvunja kingo zake Jumatano asubuhi.

Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya linasema timu zake za kukabiliana na mafuriko zinafanya kazi katika maeneo mengi yaliyoathiriwa na mafuriko, zikihamisha familia kwenye usalama na kutoa afua nyingine za kuokoa maisha.

Wakazi wa baadhi ya mashamba jijini Nairobi pia wameachwa bila makao baada ya nyumba zao kuzama kutokana na mafuriko. Mvua inatabiriwa kuendelea kunyesha.

 


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved