Huku idadi ya waliofariki katika mkasa wa mafuriko huko Mai Mahiu kaunti ya Nakuru ikizidi 50, mzee mmoja amejitokeza na kuelezea jinsi mafuriko hayo yalibisha hodi katika boma lake la kuwasomba wanawe.
Mze Grishon Waiganjoa alizungumza na BBC News na kwa masikitiko makubwa, alisimulia jinsi aliwapoteza wanawe 2 wa kiume katika mkasa huo wa mafuriko Jumapili usiku.
“Nilisikia sauti ya maji yakibubujika kwa kasi na nguvu, nilikuwa na mke wangu na wajukuu ndani ya nyumba, nikawaambia amkeni maji yameingia. Hata hatukumaliza dakika tatu, maji yalijaa hapa kote,” mzee huyu alihadithia akiwatembeza wanahabari katika boma lake lililofagiliwa na maji na kusalia tambarare.
Alisema kuwa kishindo cha maji kilikuwa kikubwa na yalianza kuingia kwa nyumba ikabidi wao kujikusanya kwenye kona moja ya nyumba na kuomba Mungu.
“Tulijikunyata kwa nyumba tukaanza kuomba, Mungu ulisema hutamaliza tena watu kwa mafuriko, tusaidie. Tukakaa tu tukiomba na sasa maji yamekuja mingi kwa nyumba. Sisi hatukujua kunafanyika nini, asubuhi ndio tuliona madhara yake namna hii,” Waiganjo alisema.
Kuamka asubuhi, alipata vitu vyake vingi vimesombwa na maji, lakini kilichomuuma Zaidi na kubaini kwamba hata wanawe pia walikuwa miongoni mwa vitu vilivyosombwa.
“Kuamka sasa mimi nashindwa nitaanzia wapi, mtoto wangu hakuna, mbuzi walienda na maji. Mtoto mmoja alitolewa hapa karibu, mwingine alisombwa na maji mpaka huko mbali baada ya Mungu kusimamisha mafuriko,” Waiganjo alisema baina ya majonzi.