Rais William Ruto alipokea ujumbe wa mshikamano kutoka kwa Mfalme Charles III wa Uingereza siku ya Jumanne huku taifa likiendelea kukumbwa na mvua kubwa na mafuriko.
Katika barua yake kwa rais Ruto, Mfalme Charles ambaye alikuwa nchini Kenya mwezi Oktoba mwaka jana alisema kuwa yeye na mkewe walikuwa na wasiwasi kuhusu mafuriko katika taifa hili na athari ambayo imekuwa nayo kwa maisha ya watu.
“Tunaweza tu kuanza kufikiria uchungu wa wale ambao wamepoteza wapendwa wao na kuona maisha yao yakiwa yameharibika. Mawazo yetu pia yako kwa wale wafanyikazi wa dharura na wengine ambao wanafanya kazi kwa muda mrefu kusaidia wale ambao wameathiriwa sana,” Mfalme Charles alimwandikia Rais Ruto.
Aliongeza, "Kuongezeka kwa hali ya kutotabirika na vurugu za mifumo ya hali ya hewa hutukumbusha jinsi ilivyo muhimu sana kwamba ulimwengu uchukue hatua pamoja na kutuma ujumbe wote ili kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kama tulivyojadili wakati wa ziara yetu nchini Kenya mwaka jana, changamoto ya mabadiliko ya hali ya anga na upotevu wa bayoanuwai inatuangukia sisi sote kushughulikia: hatarini ni ubora wa maisha na uhai wetu kama ulimwengu."
Mfalme alibainisha kuwa upendo na makaribisho mazuri ambayo yeye na mkewe walipokea wakiwa nchini Kenya mwaka jana vilimsukuma kutuma ujumbe wa mshikamano.
"Tukikumbuka kwa furaha ukaribisho tuliopokea katika ziara yangu mwaka jana, na urafiki kati ya nchi zetu mbili tulitaka kutuma huruma na mapenzi yetu ya kina kwa watu wa Kenya," aliandika.
Haya yanajiri wakati viwango tofauti vya mvua vikiendelea kushuhudiwa nchini. Mvua hizo zimekuwa na athari mbaya ikiwa ni pamoja na mafuriko, maporomoko ya ardhi, miongoni mwa mengine.