Mfanyikazi wa KQ ambaye alikuwa amezuiliwa na Kitengo cha Ujasusi cha Kijeshi cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hatimaye ameachiliwa.
Lydia Mbotela aliachiliwa baada ya kuzuiliwa kwa jumla ya wiki mbili, Katibu wa kudumu katika wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Sing'oei amethibitisha.
Kulingana na PS, Lydia Mbotela, meneja wa KQ anayefanya kazi DRC, aliachiliwa baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na Mwakilishi maalum wa Kijeshi wa Kenya na Balozi Mdogo.
Mwishoni mwa Aprili, Afisa Mkuu Mtendaji wa KQ Allan Kilavuka alithibitisha kukamatwa kwa wafanyikazi wake katika taarifa ya vyombo vya habari, akisema wawili hao walikamatwa na Kitengo cha Ujasusi wa Kijeshi huko Kinshasa kwa "kukosa hati za forodha za shehena ya thamani."
Kilavuka alikashifu mamlaka ya Kinshasa kwa kuwakamata wawili hao, akidai kuwa walishikiliwa kinyume na amri ya mahakama, na kwamba mizigo inayohusika haijachukuliwa au kukubalika na KQ.
KQ ilikuwa imesitisha safari zake za ndege hadi Kinshasha, ikisema kuwa haingeweza kutoa huduma zake ipasavyo bila wafanyikazi wake.