Mwaka 2018, João, mwenye umri wa miaka 63, alianza kugundua maumivu kwenye uume wake.
"Nilianza kutembelea kliniki ili kujua ni nini, lakini madaktari wote waliniambia ni kutokana na ngozi ya ziada na kunipatia dawa ," anakumbuka mzee huyo mwenye umri wa miaka 63.
Licha ya dawa hiyo, dawa hiyo ngozi iliendelea kuvimba.
Hii ilianza kumuathiri João na ndoa yake na mkewe hususan maisha ya ngono. "Tulikuwa kama ndugu," anakiri.
Kwa miaka mitano, João (sio jina lake halisi) alitembelea wataalamu wengi ambao walimuandikia dawa zaidi na kuagiza afanyiwe uchunguzi wa kina kubaini ni nini kinachoendelea katika uume wake. "Hakuna kitu kilichoweza kutatuliwa," alisema.
Kisha, mnamo 2023, waliweza kupata utambuzi: João alikuwa na saratani ya uume .
"Kwa familia yanguk ilikuwa kitu kibaya sana, hasa kwasababu walilazimika kukata sehemu ya uume wangu. " Nahisi kama nimekatwa kichwa," anasema.
"Ni aina ya saratani ambayo huwezi kuzungumza na watu kuihusu kwa sababu inaweza kuwa utani."
Ukweli ni kwamba saratani ya uume ni nadra, lakini matukio na viwango vya vifo vinaongezeka duniani kote.
"Hofu kuhusu upasuaji"
Kulingana na tafiti za hivi karibuni, Brazil, ambapo João anatoka, ina moja ya viwango vya juu vya saratani ya uume ulimwenguni: kuna idadi ya 2.1 kwa wanaume 100,000.
Kati ya mwaka 2012 na 2022, visa 21,000 viliripotiwa, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Brazil.
Hii imesababisha vifo vya watu 4,000 na 6,500 kukatwa uume wao katika kipindi cha miaka kumi iliyopita: mmoja kila baada ya siku mbili.
Dalili za saratani ya uume mara nyingi huanza na vidonda ambavyo haviponi na mara nyingi huwa na harufu mbaya.
Wakati utambuzi wa mapema wa ugonjwa huo unafanikiwa, kuna uwezekano mkubwa wa kupona kupitia taratibu kama vile upasuaji, na tiba za mionzi za radiotherapy au chemotherapy.
Lakini ikiwa haitatibiwa, inaweza kusababisha kukatwa kwa sehemu au uume wote kwa ujula na labda hata viungo vingine vya siri kama vile korodani.
João alilazimika kufanyiwa upasuaji wa sehemu ya uume wake mwezi Januari mwaka jana. Kwake ulikuwa ni wakati mgumu.
Sikuwahi kufikiria kwamba nitasumbuliwa na ugonjwa. Na ni kitu ambacho huwezi kumwambia kila mtu, "anafafanua.
"Niliogopa sana kuhusu upasuaji, lakini hakukuwa na njia nyingine. Hisia katika wiki za kwanza zilikuwa huzuni. Siwezi kukataa. Kuachwa bila sehemu ya uume wako ni jambo la kutisha."
Kwa wagonjwa wengine suluhisho pekee ni kukatwa kwa uume. Ni kitu ambacho kinabadilisha maisha milele.
Thiago Camelo Mourão, kutoka idara ya tiba ya uzazi ya wanaume-(urolojia) ya Kituo cha Saratani cha Sao Paulo, anasema kuwa "ikiwa kuna kukatwa kwa sehemu, mkojo unaendelea kutoka kwa uume."
"Katika kisa cha kukatwa kabisa, njia ya mkono inaweza kuhamishwa kwa sehemu ya mwili, kati ya scrotum(mfuko unaobeba mbegu za kiume) na njia ya haja kubwa, na kusababisha mgonjwa kukojoa akiwa ameketi chooni."
Inasababishwa na nini?
Kulingana na wataalamu, kuna sababu kadhaa za hatari ambazo zinaweza kusababisha saratani ya uume, kama vile phimosis - ugonjwa ambao huzuia ngozi ya uume kuondolewa - au uvutaji wa sigara.
Mauricio Dener Cordeiro, mtaalamu aliyebobea katika mada hii tiba ya uzazi wa wanaume, anasema kuwa usafi wa kibinafsi una jukumu katika ugonjwa huu.
"Wakati mtu hafunui ngozi ya uume na kutosafisha ngozi inayoizunguka vizuri, hii husababisha kutokwa na maji maji ambayo hukusanyika na kusababisha maambukizi ya bakteria," anasema.
"Ikiwa hii itatokea mara kwa mara, inakuwa sababu ya hatari ya kutokea kwa uvimbe ," anaongeza.
Lakini pamoja na usafi, Cordeiro anasema kuwa maambukizi ya mara kwa mara na virusi vinavyosababisha mahonjwa ya zinaa au Human papilloma yanaweza kuwa moja ya "sababu kuu za hatari."
Katika baadhi ya matukio, virusi vya Human papilloma vinaweza kusababisha saratani ya mdomo na uume.
"Chanjo dhidi ya virusi vya Human papilloma ni muhimu kutokana na ufanisi wake mkubwa katika kuzuia majeraha yanayohusiana na aina hii ya ugonjwa," anasema Cordeiro.