Harusi ya pamoja ya mayatima 100 nchini Nigeria imefutiliwa mbali, kufuatia wasiwasi mkubwa wa umma kuhusu ustawi wa wale waliohusika.
Harusi hiyo iliyopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, ilifadhiliwa na Abdulmalik Sarkindaji, spika wa bunge la taifa katika jimbo lenye Waislamu wengi kaskazini-magharibi mwa Niger.
Ilihusisha watoto yatima ambao walikuwa wamepoteza wanafamilia wakati wa mashambulizi ya magenge yenye silaha.
Wakosoaji wameelezea wasiwasi wao kwamba wasichana wengine wanaweza kuwa na umri mdogo au kulazimishwa kufuata sheria ili kupata faida ya kifedha.
Lakini Jukwaa la Maimamu la Niger lilisema sherehe ya ndoa itaendelea tarehe 24 Mei na kusisitiza kuwa wasichana hawakuwa na umri mdogo.
Umri wa wasichana hao haujabainika.
Waziri wa Masuala ya Wanawake wa Nigeria Uju Kennedy-Ohanenye alilaani mpango huo na kusema ataomba amri ya mahakama kusitisha sherehe hiyo.
Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Nigeria pia wamezindua ombi la kusitisha mpango huo.
Kufuatia ghadhabu hiyo ya umma, Spika Sarkindaji ametangaza kujiondoa kwenye hafla hiyo.
Baadhi ya maharusi waliokusudiwa, ambao walizungumza na vyombo vya habari vya ndani, walitetea mpango huo.
Harusi za pamoja ni jambo la kawaida katika maeneo mengi ya Waislamu kaskazini mwa Nigeria, ambapo kanuni za kidini na kitamaduni kama vile mitala zinaunga mkono mpango huo.