Rais William Ruto ameelekea Jamhuri ya Korea kuhudhuria Kongamano la Korea-Afrika, mkutano wa ngazi ya juu ambao unaahidi kuchochea uhusiano wa kina kati ya kanda hizo mbili.
Mkutano huo utatumika kama jukwaa kwa Afrika na Korea Kusini kuangazia maeneo yenye maslahi kwa pande zote, kuanzia kukuza biashara na ukuzaji wa viwanda hadi maendeleo ya miundombinu na kuunda nafasi za kazi.
Kulingana na taarifa kutoka kwa msemaji wa Ikulu,Hussein Mohamed, mijadala hiyo itaenea hadi kwenye mada muhimu kama vile uzalishaji wa kilimo, mwitikio wa mabadiliko ya hali ya hewa, na mpito kuelekea vyanzo vya nishati isiyo na kaboni.
Mazungumzo ya nchi mbili kati ya Rais Ruto na mwenzake wa Korea Kusini, Rais Yoon Suk Yeol pia yako kwenye ajenda. Viongozi hao wawili wanatarajiwa kukagua maendeleo ya ushirikiano wa shilingi bilioni 132 wa mpangilio wa mfumo uliokubaliwa wakati wa ziara ya Ruto mjini Seoul mnamo Novemba 2022.
Safari hiyo, kulingana na Ikulu, pia itazoa shilingi bilioni 25 kwa ajili ya miradi ya maji na ukulima wa umwagiliaji maji.
"Ushirikiano huu unalenga katika miradi muhimu ikiwa ni pamoja na maji na umwagiliaji, kilimo, miundo mbinu, na uchumi wa ubunifu," taarifa hiyo kutoka Ikulu ilisema.
Mikataba kadhaa ya makubaliano itatiwa saini katika ziara hiyo ili kuimarisha ushirikiano katika afya, kilimo, teknolojia ya habari na mawasiliano, miongoni mwa sekta nyinginezo.
"Kenya itashirikiana na Korea Kusini kuchunguza fursa za teknolojia, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya sekta ya viwanda," Taarifa kutoka Ikulu ilisema.
Kenya pia inatazamiwa kujiunga na taasisi ya kimataifa ya Chanjo (IVI) ili kuendeleza malengo yake ya utengenezaji wa chanjo. Katika safari hiyo, Kenya na Korea Kusini zinatarajiwa kukamilisha mpango wa uhamiaji wa wafanyakazi, ambao unaweza kuifanya Kenya kuwa miongoni mwa nchi chache za kiafrika zilizoidhinishwa kwa usambazaji wa vibarua chini ya mpango wa mfumo wa Kibali cha Ajira (EPS) wa Korea Kusini.