logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wakenya watahadharishwa kuhusu mvua na baridi kali

Milima ya magharibi mwa bonde la ufa,ziwa Victoria na maeneo ya kaskazini magharibi yatashuhudia mvua ya juu kuliko wastani

image
na Davis Ojiambo

Habari04 June 2024 - 08:16

Muhtasari


  • •Wananchi wanaagizwa kuvaa nguo za joto katika msimu wa baridi
  • • Wananchi wameonywa kuwepo kwa mafuriko katika maeneo yaliyotengwa na pia maeneo tambarare ya mafuriko 

Idara ya hali ya hewa imetoa tahadhari kwa wananchi wa Kenya kuhusu ongezeko la baridi katika maeneo ya Nairobi na Mlima Kenya.

Katika utabiri wa hali ya hewa wa miezi ya Juni, Julai na Agosti, mkugurugenzi wa idara ya hali ya hewa David Gikungu aliangazia kaunti ambazo zitaathirika zaidi ikiwemo Nairobi, Kiambu, Laikipia, Murang’a, Embu, Meru,Kirinyaga, na nyanda za chini za kusini mashariki mwa Machakos na Makueni ambazo zitakua na mawingu yakiambatana na baridi.

Vilevile,idara hiyo ilisema kuwa hata kama ni wakati wa baridi, kutakuwa na joto kiasi kuliko baridi itakayoshuhudiwa msimu huu.

“Hata kama ni kawaida ya msimu huu kuwa na baridi,kutakuwa na joto kushinda nyakati nyingine za msimu,” alisema David Gikungu, mkurugenzi wa huduma ya hali ya hewa.

Vilevile, aliwasihi wananchi na wizara ya afya kutahadhari kutokea kwa magonjwa ya kupumua kama vile Pumu, Mafua, Nimonia na mafua ya kawaida msimu huu.

“Wananchi wanaagizwa kuvaa nguo za joto na pia kukoma kutumia jiko za makaa kujikingia baridi kwani monoksidi kaboni inaweza kuwa hatari wakati inapumuliwa kwa ndani.” Aliendelea Gikungu.

Vilevile, milima ya magharibi mwa bonde la ufa,ziwa Victoria na maeneo ya kaskazini magharibi ikiwemo kaunti za Turkana, West Pokot, Baringo, Nakuru, Nyamira na Kisii yatashuhudia mvua ya juu kuliko wastani.

Fauka ya hayo, daktari Gikungu anaonya kuwepo kwa mafuriko katika maeneo yaliyotengwa na pia maeneo tambarare ya mafuriko hasa ziwa Victoria.

Hivyo basi, amewasihi serikali na wananchi kuwa makini wakati janga hili linapotokea. Pia,ameirai serikali kuwekeza mikakati kabambe ya kusetiri majanga haya.

“Mvua ya juu kushinda wastani itasaidia katika kukuza ukulima. Taasisi husika zimeagizwa kutumia mikakati dhabiti ili kudhibiti wadudu kwenye mashamba ya wakulima. Hii itapiga jeki juhudi za serikali za kukuza ukulima,” alimalizia Daktari Gikungu.

Ubashiri wa hali ya hewa unaonyesha kuwepo kwa mvua zaidi ya wastani kwenye ukanda wa pwani. Hata hivyo, wakenya wameraiwa kukuza maji ya kutosha katika maeneo kame.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved