Mwalimu katika shule moja ya upili kaitka kaunti ya Nyamira ameripotiwa kujitoa uhai baada ya kupoteza shilingi elfu 50 kwenye mchezo wa Kamari.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, marehemu ambaye alikuwa mwalimu wa shule moja ya upili kaitka kaunti hiyo alijitoa uhai usiku wa Jumatano baada ya kupoteza kitita hicho cha hela kwenye Kamari ya Aviator.
Aviator ni mchezo wa kimitandaoni wa bahati nasibu ambao mtu huweka pesa na kusubiri ‘ndege kupeperuka’ ili kuongeza nafasi yake ya kupata hela maradufu baada ya kufanya kile wanaita kwa kimombo ‘cash-out’.
Taarifa zilisema kwamba mwalimu huyo alikuwa awali ameonekana mwenye mawazo mengi na kuwafanya walimu wenzake kumkopa hadi shilingi elfu 50 akisema alikuwa na matatizo Fulani ya kuyashughulikia, lakini zote zikaishia kwenye Kamari.
Naibu chifu wa Nyamira Township, Johnson Manyara alithibitisha kisa hicho na kusema kwamba alipokea simu nyakati za usiku baada ya mwalimu huyo kupatikana amefariki.
“Nilipokea simu kutoka kwa umma kuhusu mwalimu ambaye alishukiwa kujitoa uhai. Haraka nilielekea kwa nyumba yake na kupata mwili wake. Mke wake alikuwa amesafiri kwenda kijijini baada ya kujifungua. Pia walikuwa wametaarifiwa kwamba wazazi wake walikuwa wanaumwa na alimtuma mkewe kwenda kuangalia hali zao,” Naibu chifu alinukuliwa.
Mwalimu mkuu wa shule husika alisema kwamba marehemu alikuwa ameajiriwa na uongozi wa shule kwa muda wa miaka minne mpaka kufikia kifo chake.