Watu kadhaa wanaoishi katika maeneo ya Mathare na Mukuru Kayaba wamelalamikia serikali kutokana na ukosefu wa majina yao katika ugavi wa shilingi elfu kumi kwa kila boma kutoka kwa serikali.
Wakizungumza na Nation, wengi walidai kuwa wapo wahusika wakuu ambao wametumika katika ufisadi na ugavi huo wa hela.
Akizungumza mnamo Jumapili, naibu kamishna wa kaunti John Kisang, aliamuru kuwa majina yanayokosa ya wahusika yaelekezwe katika ofisi ya South B na kisha apewe nakala ya orodha .
‘’Hatuwezi kubali haramu ikithiri katika ofisi za serikali. Tutaangalia na tuhakikishe na iwapo kuna mtu amejikita kwenye ufisadi, atakuwa na hatia’’, alisema Kisang.
Serikali ilikuwa imewaahidi kuwapa kila familia shilingi elfu kumi mbele ya ubomozi wa nyumba zilizojengwa katika maeneo ya utoaji maji kwenye sehemu za Nairobi, Ngong na vilevile Mathare.
Maswali mengi yamezidi kuchipuka kila kukicha hasa kuhusu ubomoaji unaoendelea katika maeneo ya Mathare huku baadhi ya wananchi wakisisitiza kuwa wanaambiwa watoe hongo ndipo makazi yao yasibomolewe.
Wahudumu wa taasisi ya Kenya Human Rights Commission waliowasili eneo la tukio hilo, walilalamikia kuwa, walemavu walikuwa wamesahaulika.
‘’Kuna ukosefu wa uaminifu katika ugavi wa hela na vilevile usaidizi wa waja walioathirika haufikii kwenye mikono ya PWDs,’’ alisema huku akirai serikali iwalinde kina mama na watoto.
Vilevile, mkurugenzi wa I Rise International School Bi. Susan Irungu akizungumza na Nation, alisema kuwa wabomoaji hao walikuwa wanaomba shule shilingi milioni moja ndiyo shule ibaki licha ya kupata kibali kutoka kwa wizara ya elimu.