Polisi katika eneo la Gem, Kaunti ya Siaya, wanachunguza tukio moja ambalo limewaacha wengi vinywa wazi ambapo familia moja iliwapoteza ng'ombe saba na kondoo tisa kufuatia tukio la mkasa wa moto ambao ulitokea kwenye kitongoji cha Murumba mnamo usiku wa kuamkia leo.
Wakazi wanaamini kwamba wahalifu waliteketeza kwa moto zizi la ng'ombe la familia hiyo, na kusababisha wanyama kuteketea kupindukia.
Mhudumu wa nyumba aliiambia Citizen kwamba aliamshwa na mayowe ya majirani majira ya saa kumi asubuhi na kuarifiwa kuwa zizi la ng'ombe lilikuwa likiwaka moto.
Alipowasili kwenye mkasa huo, alikuta tayari limezidiwa na moto mkali na wanyama wote ndani yake.
Kupitia msaada wa wenyeji, mhudumu alijitahidi kwa udi na uvumba kuzima moto huo ila juhudi na jitihada zao ziliambulia patupu mighairi ya mafanikio.
Vilevile, aliongeza kwamba aliweza kumuokoa kondoo mmoja peke yake.
Familia inasema kuwa wanashuku moto ulisababishwa na jirani yao ambaye amekuwa na matatizo na mhudumu huyo na kwamba wanataka uchunguzi ufanyike na jirani huyo achunguzwe.
Naibu chifu wa eneo hilo, Millicent Otieno, alilaani tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi tayari umeanzishwa kuhusu suala hilo.
Alionya kwamba washukiwa watapatikana na kufikishwa mbele ya sheria.