Jairus Onkundi Morwabe, kijana wa miaka 24 ambaye alidaiwa kimakosa kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji ya Kware amejitokeza kusafisha jina lake.
Baada ya taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatatu na maafisa wa DCI kuhusu kukamatwa kwa mshukiwa mkuu wa mauaji hayo ya kutisha, baadhi ya wanamitandao waliibua shaka kuhusu mshukiwa huyo huku wengine wakienda hatua zaidi ya kuchapisha majina na picha za kijana asiye na hatia, Jairus Onkundi, wakidai ndiye aliyetangazwa na wapelelezi kuwa mshukiwa mkuu.
Kufuatia kuhusishwa na uchunguzi unaoendelea, Onkundi ambaye ni mhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Meru alijiwasilisha kwa kituo cha polisi na kueleza jinsi alivyoshtuka baada ya kuona akihusishwa na mauaji hayo.
"Nilitembelea jukwaa la X na kupata chapisho. Nilishtuka sana kwa sababu sijawahi kuhusika katika kosa lolote la jinai wala sijawahi kukamatwa hapo awali,” Onkundi alisema.
Mwanafunzi huyo wa zamani wa sayansi ya kompyuta alisema alikuwa kazini katika mtaa wa Parklands, Nairobi wakati alipoona ripoti hizo za kupotosha. Kisha alishauriwa kutembelea kituo cha polisi kilicho karibu ili kuandikisha ripoti ili kuepusha matatizo zaidi.
Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa makosa ya Jinai, Mohamed Amin alithibitisha kuwa kijana huyo si mhalifu na kubainisha kuwa alisaidiwa kukabiliana na hali ya kutisha iliyompata.
“Tangu wakati huo, Jairus amepewa msaada unaohitajika kutoka upande wa polisi, na taarifa hii kwa waandishi wa habari inatoa fursa ya kufafanua kwa wananchi kwamba kijana huyo wa miaka 24 si mhalifu, na wala hatakiwi na polisi wala DCI kwa sababu yoyote ile,” DCI Amin alisema.
Amin pia iliwakosoa watumiaji wa mitandao ambao wanapuuza uchunguzi wao na kuweka wazi kuwa wanaufanya kikamilifu.
"Siku zote tuko makini kuhakikisha kwamba taarifa zozote zinazotoka kwetu ni za kuaminika na kuthibitishwa vyema," Amin alisema.