Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 59 amefunguka na kusimulia mkasa uliomkuta baada ya lifti kukataa kufanya kazi na kumfungia ndani kwa zaidi ya saa 40.
Akizungumza na BBC, Ravindran Nair kutoka jimbo la Kerala kusini mwa India, ambaye alikwama kwenye lifti ya hospitali kwa saa 42 bila chakula wala maji, alisema kuwa alihofia angefia humo.
Mwanamume huyo aliingia kwenye lifti ya hospitali kukutana na daktari Jumamosi mchana - kisha akabaki amekwama ndani hadi Jumatatu asubuhi, wakati mkarabati wa lifti alipomkuta akiwa hoi.
Sasa yuko hospitali na anatibiwa upungufu wa maji mwilini na maumivu ya mgongo.
Watu wa familia yake hapo awali walidhani alikuwa kazini, lakini baadaye waliwasiliana na polisi na kuanza msako mkali wa kumtafuta.
Tukio hilo limegonga vichwa vya habari, na kusababisha serikali ya jimbo hilo kuwasimamisha kazi mafundi watatu na kuanzisha uchunguzi.
Bw Nair aliambia BBC kwamba aliponaswa, alijaribu kupiga nambari ya dharura iliyoorodheshwa kwenye lifti lakini hakujibiwa.
Pia alijaribu kumpigia simu mke wake Sreelekha CP, ambaye anafanya kazi hospitalini, na "mtu mwingine yeyote ambaye ningeweza kumfikiria", lakini simu hazikuweza kuunganishwa.
"Nilianza kuogopa na kuanza kugonga milango ya lifti ili kuvutia watu. Hapo ndipo simu yangu ilipoanguka sakafuni na kuacha kufanya kazi," alinukuliwa.
"Nilipiga kelele na kupiga mayowe kuomba msaada na nilijaribu kung'oa milango kwa mikono yangu. Sasa kulikuwa na giza ndani ya lifti, lakini cha kushukuru, kulikuwa na hewa ya kutosha ya kupumua."
Kisha akazunguka kwenye lifti, akibonyeza kengele ya hatari tena na tena, akitumaini kwamba ingelia na kuvutia umakini wa mtu - lakini bila mafanikio yoyote.
“Saa zilizidi kwenda sikujua ni mchana au usiku kwani ndani kulikuwa na giza totoro, nilipochoka nililala pembeni, ikabidi nitumie kona nyingine kujisaidia haja zote,” anasema.
Kwa kawaida anapotembelea hospitali yeye na mkewe hutumia lifti iliyotengewa wafanyakazi. Lakini wakati huu aliingia katika Lift-11 - iliyokusudiwa kwa wagonjwa na wageni - kuelekea ghorofa ya pili.
"Ilikuwa tu saa sita mchana basi. Hakukuwa na mtu mwingine kwenye lifti lakini taa ilikuwa imewaka, kwa hivyo sikufikiria kuwa kuna kitu kibaya," anasema.
Akabonyeza kitufe na lile lifti ikaanza kupanda lakini ilipokaribia ghorofa ya pili, ilishuka chini kwa kishindo na kukwama kati ya ghorofa ya kwanza na ya pili.
Hakujua basi kwamba mateso yake yangedumu karibu siku mbili.