Rais wa Uganda ,Yoweri Kaguta Museveni, ameungana na mwenzake wa Kenya William Ruto kuwashutumu wageni kutoka nje ya nchi kwa kufadhili maandamano.
Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Museveni ambaye amekuwa mamlakani tangu 1986 aliwapongeza Waganda kwa kutoshiriki maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumanne akisema walikuwa na vipengele viwili vya kutupiliwa mbali.
Alidai kuwa baadhi ya wakoloni mamboleo walikuwa wakifadhili maandamano hayo na kwamba wanaopanga mipango hiyo walikuwa na nia mbaya.
“Mambo mabaya sana, yatatoka mahakamani wakati waliokamatwa watakapofunguliwa mashtaka. Inawezekana, kwamba baadhi ya washiriki, hawakujua kuhusu fedha zilizopangwa kutoka nje na mambo mabaya yaliyopangwa. Ndio maana, walipaswa kusikiliza ushauri wa polisi, sio kuendelea na maandamano. Lakini walipuuza ushauri wa polisi,” Museveni alisema Alhamisi.
Aliendelea kudai kuwa iwapo maandamano hayo yangekuwa na lengo la kweli la kupiga vita ufisadi, angejiunga na waandamanaji.
"Hakika, katika mwaka wa 2019, Nakalema alitupanga na tulitembea kutoka Square ya jiji kupitia Barabara ya Kampala hadi Jinja Road na kwenda Kololo. Watu wengi sana walikuwepo- Maaskofu, Askari, Wanainchi, n.k.
Nilifikiri kwamba Nakalema alikuwa amepanga siku ya Jumapili kwa sababu hapakuwa na trafiki, wala watembea kwa miguu barabarani. Nakalema sasa ameniambia, kwamba ilikuwa Jumatano, tarehe 4 Desemba, 2019, lakini walikuwa wamejipanga na polisi kuzuia trafiki kwa saa kadhaa,” alisema.
Rais alibaini kuwa kukamatwa kwa watu hao kulitokana na operesheni ya hali ya juu ya kijasusi akisema yeye ndiye aliye na habari nyingi.