logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mvua ya damu ni nini na husababishwa na nini?

Mvua ya damu kwa kawaida hutokea wakati mkusanyiko mkubwa wa vumbi jekundu linapochanganyika na mvua.

image
na Samuel Maina

Habari28 July 2024 - 11:32

Muhtasari


  • •Mvua ya damu kwa kawaida hutokea wakati mkusanyiko mkubwa wa vumbi jekundu linapochanganyika na mvua.

Mara tu tunaposikia neno mvua, tunafikiria maji yanayotoka angani, lakini wakati mwingine vitu vingine visivyokuwa maji pia huanguka kutoka angani na kuna sababu za kimazingira.

Inaweza kushangaza lakini 'mvua ya damu' ipo. Neno mvua ya damu hutumiwa pale maji yenye rangi nyekundu yanaponyesha kutoka angani.

Sababu ya mvua ya damu

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya hali ya hewa ya Met Office ya Uingereza, mvua ya damu si neno kutoka kwa wataalamu wa hali ya hewa na wala sio la kisayansi, lakini ni neno tu la kawaida la mazungumzo.

Mvua ya damu kwa kawaida hutokea wakati mkusanyiko mkubwa wa vumbi jekundu linapochanganyika na mvua. Kutokana na hilo, rangi ya mvua huonekana nyekundu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Met Office, mvua ya damu husababishwa na upepo mkali au dhoruba ambao hubeba vumbi. Vumbi hili hutawanywa angani na linaweza kusafiri maelfu ya kilomita kutokana na mzunguko wa angahewa.

Hatimaye vumbi litaanguka kutoka angani kwa sababu ya graviti au kunasa katika mawingu ya mvua na kuchanganyika na matone ya maji. Ndipo, mvua inaponyesha, matone ya mvua huonekana kuwa mekundu.

Matukio ya mvua ya damu

Mvua ya damu, ambayo matone ya mvua yanaonekana mekundu kabisa, ni nadra sana, kwani aina hii ya mvua inahitaji kiwango cha juu sana cha vumbi jekundu.

Hata hivyo, mwaka 2001, jimbo la kusini mwa India la Kerala lilipata mvua ya damu ya vipindi wakati wa msimu wa monsuni, ambayo pia ilichafua nguo. Katika monsuni hiyo hiyo, pia kulikuwa na ripoti za rangi nyingine za mvua, ikiwa ni pamoja na kijani na njano.

Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya habari ya Quint, wilaya za Kottayam, Idukki na Wayanad huko Kerala ziliripoti pia mvua nyekundu ya damu mwaka 1896, 1957, 2001 na 2012.

Kwa mujibu wa ripoti ya BBC, baada ya kutafiti hili, taarifa zilizopatikana zinaonyesha mvua hiyo ilikuwa na rangi nyekundu kutokana na vumbi lililopeperushwa na upepo mkali kutoka penisula ya Arabuni.

Lakini mvua hii inabidi inyeshe kwa muda mfupi tu, ili uweze kupata mabaki mekundu.

Mtaalamu wa hali ya hewa Philip Eden anasema, “sababu kuu nyuma ya jambo hili ni kwamba ikiwa mvua ni ya muda fupi basi kiwango cha vumbi jekundu kitakuwa kikubwa. Kwa upande mwingine, ikiwa kuna mvua kubwa na ya muda mrefu, mabaki ya vumbi yatasombwa na maji.”

Mvua ya damu katika historia

Mvua ya damu pia imetajwa katika historia - katika mashairi ya kale ya Kigiriki, yaliyoandikwa katika karne ya nane.

Mvua ya damu wakati huo ilionekana kama ishara ya kutabiri jambo fulani. Mwandishi wa karne ya 12 Geoffrey of Monmouth, pia alitaja mvua ya damu. Mwanahistoria wa karne ya 12 William of Newburgh, vilevile alitaja mvua ya damu.

Hapo awali, iliaminika kuwa umwagaji wa damu halisi utatokea. Mvua ya damu imetajwa mara nyingi katika fasihi na maandishi kama ishara ya 'tukio baya.'

Baada ya kukuwa na kuenea kwa sayansi katika karne ya 17, sababu za mvua nyekundu zilianza kueleweka. Karne ya 19 nadharia ya kwamba mvua hiyo husababishwa na vumbi ilienea.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved