Mbunge wa Laikipia Mashariki, Festus Mwangi Kiunjuri, hatimaye amejibu madai ambayo yamekuwa yakienezwa mtandaoni katika siku za hivi majuzi kwamba binti yake aliwasha moto uliosababisha vifo vya wanafunzi kadhaa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi mnamo 2017.
Katika taarifa aliyotoa Julai 28, waziri huyo wa zamani wa ugatuzi alipuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa msichana aliyeshutumiwa kufanya kitendo hicho si bintiye.
Wakati akijitenga na madai hayo, mwanasiasa huyo aliweka wazi kwamba hajawahi kuwa na binti au mtu mwingine wa familia aliyesoma katika Moi Girls, ambako kisa hicho cha kusikitisha kilitokea miaka saba iliyopita.
"Ningependa kurejelea taarifa yangu ya 2017 kuhusu hilohilo. Ifahamike kwa wahusika wote wa uwongo huu wa kizembe, usiojali na wa kinyama kwamba SIJAWAHI kupata binti au jamaa katika Moi Nairobi Girls,” Mwangi Kiunjuri alisema katika taarifa.”
Aliongeza, "Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu wazembe wameamua kupata alama zozote kwa kurudisha uwongo huu bila kuwazingatia wazazi na jamaa waliopoteza wapendwa wao katika tukio hilo na majeraha ambayo bado wanayo. Hii ni ya chini sana hata kwa malengo ya kupata alama za kisiasa."
Kiunjuri alieleza huruma zake kwa wazazi waliopoteza watoto wao katika kisa hicho na kusikitika kuwa makovu mioyoni mwao yamefunguliwa na watu wanaompigania kisiasa.
Pia alibainisha kuwa wazazi halisi wa mshukiwa ambaye alishtakiwa na kufikishwa katika Mahakama Kuu ya Kenya mbele ya Jaji Stella Mutuku kwa kuwasha moto ulioua wasichana 10 katika bweni la Moi Nairobi Girls wanajulikana na akawataka wanaofuatilia kesi hiyo watafute ukweli.
"Ubinadamu na maadili vilipaswa kuzingatia maumivu yao lakini hii pia imeshindwa. Hatimaye, wazazi wa msichana husika wanajulikana. Ikiwa wanaofuatilia hadithi hii wanajali ukweli, waache watembelee shule iliyotajwa na kupata ukweli wote,” alisema.
Mshtakiwa halisi alikuwa na umri wa miaka 14 wakati wa tukio hilo.
Alikuwa akilala katika bweni la Kabarnet, katika shule ya wasichana ya Moi, ambapo moto ulizuka baada ya wanafunzi kurejea shuleni kutoka likizo.