Mwenyekiti anayeondoka wa chama cha ODM, ambaye pia alikuwa mbunge maalum John Mbadi amevutia maoni mseto baada ya kudai kwamba vyama vya ODM na UDA havina tofauti kifilosofia.
Akizungumza Ijumaa jioni wakati alitokea mbele ya kamati ya bunge inayowapiga msasa mawaziri wateule, ambako jina lake lilipendekezwa na rais Ruto wiki mbili zilizopita kuchukua nafasi ya Njuguna Ndung’u katika wizara ya fedha na mipango ya kitaifa, Mbadi alisema kwamba vyama hivyo vyote licha ya kutofautiana katika masuala mbalimbali lakini vyote bado vinapigia debe makuzi ya kijamii.
Akimjibu mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed aliyeibua swali hilo, Mbadi alisema;
“Bottom up economic transformation agenda, acha nimwambie mheshimiwa Junet kupitia kwako Bwana Spika kwamba Bottom Up ni dhana ya UDA ndani ya Kenya Kwanza. Lakini ukweli ni kwamba filosofia ya UDA na ODM hakuna tofauti, kusema ukweli vyama vyote viwili ni vya kidemokrasia ya jamii,” Mbadi alisema.
Madai yake kwamba pande zote mbili kimsingi zinatetea demokrasia ya kijamii yaliwashangaza wengi.