Sehemu ya viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya imethibitisha mipango ya kuunda chama kipya cha kisiasa kilicho na lengo la kuwa na mwelekeo tofauti na serikali pana iliyotangazwa hivi majuzi na Rais William Ruto.
Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, alifichua hayo alipokuwa katika Kaunti ya Kiambu, na kuongeza kuwa kuundwa kwa chama hiki kipya cha kisiasa kumepata baraka za Rais wa mstaafu Uhuru Kenyatta.
“Jiunge na harakati mpya tunayozindua. Usifanye makosa, Rais wa zamani Uhuru Kenyatta yuko pamoja nasi,” alisema Kalonzo katika jitihada zake za kuhamasisha wakazi wa Mlima Kenya kuunga mkono chama kitakachotangazwa baadaye.
Katika kampeni yake, makamu wa rais huyo wa zamani pia anawaahidi wananchi wa eneo la Kati ya Kenya kwamba Azimio itapinga mipango yoyote ya kumng’oa Naibu Rais Rigathi Gachagua kutoka wadhifa wake.
Kundi lililoongozwa na Kalonzo ambalo pia lilijumuisha Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee, Jeremiah Kioni na kiongozi wa DAP Kenya, Eugene Wamalwa, wanaamini kuwa ni wakati wa kuondoka kutoka Azimio baada ya Chama cha ODM cha Raila Odinga kukubaliana kufanya kazi na utawala wa Rais William Ruto.
Baadhi ya washirika wa Odinga wamependekezwa na Ruto kuhudumu katika Baraza lake la Mawaziri na sasa wanangojea kuidhinishwa na wabunge kabla ya kuanza kazi.
“Mwenye tumeachiwa sasa na mwenye tunatembea naye kwa sababu lazima kuwe na mbadala wa mambo yanayofanyika katika nchi hii ni Kalonzo.
Sisi wakazi wa eneo hili (la Mlima Kenya) tufungue macho. Sisi tukitembea na Kalonzo tunaomba Mungu mapenzi yake yafanyike,” alisema Jeremiah Kioni wa Chama cha Jubilee.
“Mheshimiwa Kalonzo Musyoka, wewe ongoza sisi wote turudiane, tutengeneza ile GEMA ya mbeleni,” aliongeza aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu.