Akizungumza siku ya Jumatatu, Agosti 8, Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii alisema sherehe ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika Alhamisi, Agosti 8, 2024, sasa itafanyika Alhamisi, Agosti 15, 2024.
Bii alibainiasha kuwa mawasiliano kutoka Ofisi ya Rais yalipendekeza kwamba upandishaji wa hadhi huo uhairishwe.
“Kufuatia mawasiliano kutoka Ofisi ya Rais, utoaji wa hadhi ya mji kwa Manispaa ya Eldoret umeahirishwa kwa wiki moja kutoka Agosti 8, 2024, hadi Agosti 15, 2024.
Nawaomba sote tuendelee kushirikiana na serikali ya kaunti yetu kufanikisha tukio hili kubwa na la kihistoria,” alisema Gavana Bii.
Rais William Ruto anatarajiwa kukabidhi hati ya mji kwa Gavana Bii katika sherehe itakayofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Eldoret.
Mara hadhi hiyo itakapokabidhiwa, Eldoret itakuwa mji wa tano nchini kupandishwa hadhi baada ya Nairobi, Mombasa, Kisumu, na Nakuru.
Nakuru ilipewa hadhi ya mji mnamo mwaka wa 2021 chini ya utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Gavana Bii alisisitiza kwamba safari ya kuipa Eldoret hadhi ya mji ilianza kitambo na ilipitia hatua zote za kisheria huku manispaa hiyo ikikidhi mahitaji yote.
“Utawala wangu umekuwa ukifanya kazi kwa bidii kuhakikisha kila kipande cha tukio hili la kihistoria kinatekelezwa kwa usahihi, ikiwa ni pamoja na ushirikiano na wadau wengine na jamii ya biashara kupitia Maonesho ya MSME,” Bii aliongeza.