Waziri mpya wa Biashara Ndogo, Ndogo kabisa na za Kati (MSMEs) Wycliffe Oparanya ameapa kujiuzulu ikiwa serikali ya Kenya Kwanza itapuuza mapendekezo yake.
Akizungumza siku ya Jumapili wakati wa ibada ya kanisa katika eneo la Magharibi, gavana huyo wa zamani wa kaunti ya Kakamega alibainisha kuwa serikali inayoongozwa na rais William Ruto ilimtafuta ikitaka awasaidie kuendesha nchi.
Aliweka wazi kuwa yuko tayari kuisaidia serikali lakini kwa masharti ya kwamba inazingatia mikakati anayopendekeza.
“Hawa wameangalia, wakaangalia, wameona huyu mzee anaweza kusaidia kazi. Nitawasaidia, lakini nikiwaambia tuende njia hii na wanakataa, mimi nitajiondoa, na nirudi kwangu,” alisema.
Mwanasiasa huyo mkongwe alibainisha kwamba ni lazima mtu akubali kusaidiwa kila anapoomba msaada.
“Lazima ukubali kusaidiwa. Lakini tukiwa hapo na wewe alafu unajifanya mjuaji, tutakuwa na shida,” alisema.
Hisia za Oparanya zinakuja siku chache tu baada ya yeye, na mawaziri wengine kumi na wanane kuapishwa katika wizara tofauti.
Mawaziri hao ambao waliteuliwa baada ya rais Ruto kuvunja baraza lake la mawaziri walikula kiapo asubuhi ya Alhamisi katika Ikulu.
Siku ya Jumatano, Wabunge katika Bunge la Kitaifa waliidhinisha uteuzi wao isipokuwa Stella Langat ambaye aliteuliwa katika wizara ya Jinsia.
Waliokula kiapo ni pamoja na Aden Duale (Mazingira), Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani), Alice Wahome (Ardhi), Alfred Mutua (Kazi), Salim Mvurya (Biashara), Justin Muturi (Utumishi wa Umma), Soipan Tuya (Ulinzi) na Kipchumba. Murkomen (Michezo).
Davis Chirchir (Barabara na Uchukuzi) Rebecca Miano (Wanyamapori na Utalii), Debra Barasa (Afya), Migosi Ogamba (Elimu), Andrew Mwihia (Kilimo na Maendeleo ya Mifugo) na Eric Muuga (Maji, Usafi na Umwagiliaji), Margaret Nyambura (TEHAMA) ), John Mbadi (Hazina ya Kitaifa), Opiyo Wandayi (Nishati), Hassan Joho (Madini) na Wycliffe Oparanya (Ushirika).