Thailand imetangaza kisa chake cha kwanza kilichothibitishwa cha aina mpya ya Mpox – inayodhaniwa kuwa mbaya zaidi, cha kwanza barani Asia na cha pili nje ya Afrika.
Kulingana na Idara ya Udhibiti wa Magonjwa ya Thailand, mwanamume huyo wa Ulaya mwenye umri wa miaka 66 aliyeambukizwa aliwasili Bangkok kutoka nchi isiyojulikana ya Kiafrika mnamo tarehe 14 Agosti.
Alianza kuonyesha dalili siku iliyofuata, na mara moja akaenda hospitali. Imethibitishwa kuwa Mpox, na aina inayojulikana kama Clade 1b.
Ugonjwa huu umesababisha mlipuko wa Mpox - ambao hapo awali ulijulikana kama monkeypox - ambao tayari umeua takriban watu 450 wakati wa mlipuko wa awali katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.