Mwanahabari na mtaalamu wa mikakati ya kidijitali Dennis Itumbi ametoa shukrani zake kwa Rais William Ruto kufuatia uteuzi wa hivi majuzi wa kuitumikia serikali.
Rais Ruto mnamo Ijumaa alifanya teuzi tatu muhimu, ukiwemo ule wa Itumbi ambaye alipewa mamlaka ya Mkuu wa Uchumi wa Ubunifu na Miradi Maalum.
Akizungumza kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii siku ya Jumamosi, mwandani huyo wa rais pia aliwashukuru Wakenya kutokana na maoni yao kuhusu uteuzi huo.
“Nasikiliza mawazo yenu.. Asanteni sana kwa maneno mazuri na ukosoaji pia. Asante Rais William Samoei Ruto kwa nafasi ya kuendelea kuhudumu. Mbarikiwe na muwe na wikendi njema,” Itumbi alisema Jumamosi asubuhi.
Mwanahabari huyo mwenye utata alikuwa miongoni mwa wandani watatu wa rais walioteuliwa kuchukua nyadhifa mbalimbali muhimu serikalini.
Mawasiliano ya teuzi hizo yalifanywa na mkuu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Felix Koskei.
"Katika kutekeleza jukumu kubwa alilopewa, Mkuu wa Nchi na serikali, Mheshimiwa Rais, leo amefanya uteuzi ili kuongeza wafanyakazi wanaounga mkono utekelezaji wa Ajenda ya Uchumi ya Chini Juu (BETA)," Bw Koskei alisema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.
Kuhusu uteuzi wa Itumbi, Bw Koskei alisema, ""Uteuzi huu utaenda katika kukuza ari ya utawala huu wa uvumbuzi na ukuaji kuelekea sekta iliyoimarika na bado mpya katika nyanja ya kiuchumi."
Rais Ruto pia alimteua aliyekuwa waziri Moses Kuria wa Utumishi wa Umma kuwa mshauri mkuu katika Baraza la Washauri wa Kiuchumi.
Bw Koskei, alisema uteuzi huo unalenga kuimarisha utekelezwaji wa mpango wa Ajenda ya Uchumi ya Chini-Up na serikali yenye msingi mpana.
Kwa upande mwingine, aliyekuwa Waziri wa ICT Eliud Owalo aliteuliwa kuwa Naibu Mkuu wa Wafanyakazi, Usimamizi wa Utendakazi na Uwasilishaji.
Owalo atawajibika kwa utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ifaayo ya miradi ya kipaumbele na mipango ya utawala wa 5 kulingana na Mpango wa BETA.