logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Waziri wa mazingira kaunti ya Nairobi afichua kuchukua hatua kwa kuku aliyesumbua majirani kwa kelele

“Sasa unataka uniambie mimi ninyamaze nisiende kusaidia watu? Kama serikali sharti uchukue hatu" alisema.

image
na MOSES SAGWEjournalist

Habari23 October 2024 - 10:08

Muhtasari


  • “Sasa unataka uniambie mimi ninyamaze nisiende kusaidia watu? Kama serikali sharti uchukue hatu," Mosiria alisema.
  • Mosiria alisema kwamba wengi huenda wakaliona kama jambo dogo lakini kwa jirani mlalamishi ni bughudhi kubwa.

Waziri wa mazingira katika kaunti ya Nairobi, Geoffrey Mosiria amefichua kwamba kila siku huwa anapokea simu za malalamishi kutoka kwa wakaazi wa jiji wanaolalamikia usumbufu mbalimbali wa kelele.

Akizungumza na mtengenezaji maudhui 2Mbili, waziri huyo mchapakazi alifichua kisa kimoja ambacho kilimbidi achukue hatua licha ya kuonekana kuwa kisa kidogo.

Alielezea kwamba wakati mmoja alipokea simu kutoka kwa mkaazi wa mtaa mmoja Nairobi akilalamika kuhusu kuku wa jirani yake ambaye alikuwa anazua usumbufu wa kelele.

Mosiria alisema kuwa jirani huyo alilalamika kuwa kuku wa jirani yake alikuwa anawika kila baada ya sekunde 10, na ilimbidi afike katika mtaa huo ili kuchukua hatua.

“Mtu amelalamika kwamba kuku wa jirani yake anampigia kelele, mpaka akanitumia video, kuku huyo anawika kila baada ya sekunde 10."

"Sasa sisi kama serikali ni sharti tuchukue hatua kwa sababu haya ni malalamishi halali. Anapata usumbufu na ujue kuna sehemu ambazo hakuruhusiwi kufugwa kwa wanyama kama hao,Mosiria alieleza.

Mosiria alisema kwamba wengi huenda wakaliona kama jambo dogo lakini kwa jirani mlalamishi ni bughudhi kubwa.

“Ilibidi nichukue hatua kusuluhisha malalamisho hayo ya uchafuzi wa kelele kwa sababu jirani hangeweza kulala. Unaweza ukaliona kama jambo dogo lakini kwa watu wengine ni tatizo kuu. Mimi nina furaha kwamba tuliweza kusuluhisha hilo jambo, tulienda tukaangalia, mwenye kuku akakubali akasema atatafuta suluhu,” alisema.

Waziri huyo alieleza kuwa amepokea malalamishi ainati si tu ya uchafuzi wa kelele bali pia uchafuzi wa hewa, akitolea mfano jirani aliyelalamikia jirani mwenza mfugaji wa nguruwe waliokuwa wanafanya mazingira yao kunuka kama jalala.

Alisema kwamba kwa kuchukua hatua kutafutia suluhu matatizo hayo, si kwamba ana ujeuri bali anafanya kazi ya serikali kuwapa wakaazi mazingira bora ya kuishi.

“Sasa unataka uniambie mimi ninyamaze nisiende kusaidia watu? Kama serikali sharti uchukue hatu, hivyo si kwamba nina ujeuri bali tunafanya tu kazi kisheria,” Waziri Mosiria alisisitiza.

Kauli yake inajiri saa chache baada ya waziri wa mazingira katika serikali ya kitaifa, Adan Duale kutoa agizo kwa NEMA kufanya kazi kwa uadilifu ili kukomesha uchafuzi wa aina yote wa mazingira.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved