Rais William Ruto ameonekana kutupa kijembe kwa aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua kuhusu kujisahau katika majukumu yake kwa taifa na Wakenya.
Akitoa hotuba yake ya kumkaribisha Kithure Kindiki kama naibu mpya wa rais anayechukua nafasi ya Gachagua aliyebanduliwa, Ruto alimsisitizia Kindiki kutosahau majukumu yake.
Kiongozi wa taifa alisema kwamba viongozi hawako katika madaraka yao kuhudumia familia zao wala vijiji wanakotoka bali kuhudumia wananchi wote na taifa kwa jumla.
“Kama ambavyo niliwaambia PSs, na kama ambavyo niliwaambia CSs na vile vile ninavyowaambia kila mmoja anayefanya kazi katika ofisi ya umma, acha tufanye kazi kwa wananchi wa Kenya na taifa kwa jumla,” Ruto alisema.
“Hatuko hapa kujihudumia, au kuhudumia familia zetu, au maeneo tunakotoka au vijiji vyetu. Tuko hapa kufanyia taifa la Kenya kazi na wananchi wake.” Ruto alimsisitizia Kindiki kufanyia wananchi kazi kama ambavyo alivyosema wakati wa kula kiapo.
“Na acha niseme hivi kwamba nimekusikia kwa hakika wakati ulikula kiapo chako, umesema kwamba utahudumia watu wa Kenya na taifa la Kenya. Abra K tafadhali, fanyia watu wa Kenya kazi na taifa la Kenya,” Ruto alisema.
Ikumbukwe Gachagua alibanduliwa ofisini kwa mashtaka 11, moja ya mashtaka hayo likiwa lile la kudai serikali ya Kenya Kwanza ni kama kampuni yenye hisa.
Gachagua pia alijipata pabaya baada ya kusikika akiwatetea watu wa Mt Kenya pekee hali ya kuwa yeye alikuwa naibu rais wa taifa zima.
Gachagua alinukuliwa mara si moja akisema kwamba serikali ya Kenya Kwanza ilikuwa na hisa kwa wenye waliwapigia kura tu, kauli ambayo baadae ilikuja kumtia katika tanuru la moto kwenye bunge la kitaifa na seneti kupelekea kung’atuliwa kwake ofisini.