Msomi wa kisheria, profesa Kithure Kindiki anatarajiwa kuapishwa leo hii kuanzia majira ya saa nne asubuhi kama naibu rais mpya.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyochapishwa kwenye gazeti la serikali usiku wa Alhamisi, Kindiki ataapishwa katika ukumbi wa KICC, akichukua nafasi ya Rigathi Gachagua aliyebanduliwa ofisini.
Kuapishwa kwa Kindiki kunajiri saa chache baada ya jopo la majaji watatu katika mahakama kuu kuondoa amri ya kuzuia kuapishwa kwake Alhamisi alasiri.
Katika kisa cha kisiasa ambacho hakijawahi kushuhudiwa ambacho kimekumba Kenya, Rigathi Gachagua aliondolewa afisini wiki mbili zilizopita baada ya bunge kuidhinisha kwa wingi hoja ya kumtimua.
Rais William Ruto mara moja alimteua Kindiki ambaye mpaka kuondolewa kwa amri ya kuzuia kuapishwa kwake alikuwa waziri wa mambo ya ndani kuchukua nafasi ya Gachagua.
Lakini naibu huyo wa rais aliyetimuliwa alienda kortini akipinga kuondolewa kwake akitaja kuwa ni mambo ya kisiasa.
Bunge lilikuwa limeidhinisha uteuzi wa Kindiki lakini mahakama ilisimamisha kuapishwa kwake ikisubiri changamoto za kisheria kutoka kwa Gachagua na wengine.
Baada ya taarifa kuwekwa wazi kwamba Kindiki ataapishwa kama naibu rais, Ruto alimteua waziri mwenye mamlaka makuu, Musalia Mudavadi kushikilia majukumu ya waziri wa masuala ya ndani kikaimu.