WAKILI Ahmednasir Abdullahi amemshauri rais William
Ruto kufungua macho yake na kuangalia katika picha pana ya tatizo kuu
linalosumbua nchi.
Kupitia ukurasa wake wa X, Ahmednasir alisema kwamba
rais Ruto amejikita katika kutatua masuala anayofikiria kuwa ndiyo shida kuu ya
Kenya bali ni matatizo tu yanayochukua asilimia moja tu ya shida za Kenya.
Kwa mujibu wa wakili huyo, shida kuu ya Kenya ni
ufisadi na wizi wa mali ya umma.
Ahmednasir anahisi kwamba ikiwa taifa litafanikisha
kutatua tatizo la ufisadi, hapo litakuwa limemaliza shida za Kenya kwa asilimia
99.
“Tatizo
la namba 1 la Kenya NI UFISADI na WIZI wa FEDHA ZA UMMA...kila kitu kingine ni
maneno madogo madogo. REKEBISHA UFISADI, na utakuwa umerekebisha 99% ya
matatizo ya Kenya,” Ahmednasir alisema.
Aidha, wakili huyo alisema kuwa masuala mengine
ambayo rais Ruto yuko katika mstari wa mbele kuyatekeleza sasa hivi, japo ni
mengi lakini yote kwa jumla yanatatua shida za Kenya kwa asilimia 1 tu!
Alisema kuwa miradi kama ya kufanikisha bima mpya ya
afya, SHA,ujenzi wa viwanja vya michezo, kupanda miti bilioni 10, kujenga
barabara na mengine ni shida ndogo ndogo tu.
“Shughulikia
maneno madogo madogo (yaani, nyumba za bei nafuu, SHIF, barabara, mabwawa,
mtindo wa fedha wa vyuo vikuu, mtindo wa kugawana mapato, sodo, chanjo ya
ng'ombe, kupanda miti milioni 10, kujenga viwanja 50, bei ya unga ni kshs 110,
kuvutia 2.5 m watalii wa kigeni, mikataba ya utendakazi...n.k) na
unashughulikia 1% ya matatizo ya Kenya.
Chaguo ni rahisi. Matokeo yake ni ya kutikisa ardhi,”
wakili alishauri.
Kauli yake inajiri siku moja baada ya rais Ruto
kuongoza baraza lake la mawaziri kutia wino mikataba ya utendakazi katika ikulu
ya Nairobi.
Rais Ruto alisema kwamba mikataba hiyo itakuwa
inarejelewa kila baada ya mwisho wa mwaka wa kifedha kama njia moja ya
kufanikisha ajenda yake ya maendeleo na utendakazi kwa wananchi waliomchagua.
Haya yanajiri wakati ambapo kiongozi wa taifa
anashambuliwa kwenye mitandao ya kijamii na Wakenya wa matabaka mbalimbali kwa
kile wanamtuhumu kuwa ni kushindwa kufanikisha ajenda alizowaahidi kwenye
manifesot yake mwaka 2022.