Utafiti mpya umebaini jinsi wafanyibiashara wa pombe
wanawashawishi vijana kujitosa katika unywaji kwa kubuni majina ya kuvutia ya
aina za pombe mbalimbali.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Shule ya Sayansi ya Afya
ya Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, imefichua jinsi ushawishi wa majina
ya chapa za pombe yanavutia kwa vijana.
Hii ni licha ya serikali mbalimbali haswa ukanda wa
Afrika Mashariki kuzidisha vita dhidi ya pombe haramu za kuuzwa mitaani kwa
njia za kimagendo.
Licha ya kuondolewa kwa mifuko ya pombe maarufu kama
sachet sokoni, ripoti hiyo inaangazia kuhama kwa chupa ndogo, ambazo sasa
zinauzwa kwa wanywaji wa umri mdogo, haswa nchini Uganda.
Kulingana na utafiti wa miaka miwili uliofanywa kati
ya Juni 2022 na Novemba 2024 katika wilaya za Gulu na Wakiso, chupa ndogo, kwa
kawaida 200ml au chini ya hapo, zinauzwa kwa bei ya chini sana.
Inashangaza kwamba bidhaa hizi zinatengenezwa na
makampuni ambayo hayajasajiliwa yanayofanya kazi kinyume cha sheria, hasa
vijijini.
Profesa Nazarius Mbona Tumwesigye kutoka Shule ya
Afya ya Umma ya Chuo Kikuu cha Makerere alisisitiza kwamba kuenea kwa unywaji
pombe kumezidisha mzigo katika mfumo wa afya watu wengi barani Afrika.
Utafiti huo uliangazia kuongezeka kwa magonjwa
yasiyoambukiza yanayohusishwa na unywaji pombe, na kuweka mkazo zaidi kwenye
rasilimali za afya ya umma.
"Mwelekeo
unaokua wa matumizi mabaya ya pombe ni janga la afya ya umma, na kuchangia kwa
kiasi kikubwa kuenea kwa magonjwa yanayohusiana na pombe,"
alisema Prof Tumwesigye.
Uganda inashika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa
matumizi ya pombe kwa kila mtu, na wastani wa lita 12.21 zinazotumiwa kila
mwaka kwa kila mtu.