Mamlaka ya kitaifa ya barabara kuu nchini KeNHA imetangaza kutatizika kwa shughuli za uchukuzi katika barabara ya Mombasa Road jijini Nairobi kwenye sehemu ya kati ya mzunguko wa uwanja wa kitaifa wa Nyayo na kubadilisha barabara ya Museum Hill.
Uchukuzi utatatizika kwa saa chache mnamo Jumapili tarehe 1 mwezi Disemba ili kupisha mbio za kilomita 21 zitakazofanyika kuadhimisha siku ya ugonjwa wa Ukimwi duniani.
Kwenye taarifa yake, KeNHA imesema kwamba barabara hiyo itasalia kufungwa katika maeneo ya mzunguko karibu na uwanja wa Nyayo na Museum Hill Interchange kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi mwendo wa saa nne unusu.
Hata hivyo, wasafiri wameshauriwa kutumia njia mbadala kuendelea na safari kwa kuzingatia mwelekeo ambao umetolewa pamoja na kushirikiana na maafisa wa polisi na maafisa wa trafiki watakaowekwa kwenye sehemu hizo.
Baadhi ya barabara jijini Nairobi zitakazotumiwa kwa ajili ya riadha hizo za kilomita 21 ni ikiwemo Muindi Mbigu, Wabera, Taifa Road, Harambee avenue, Parliament Road, Haile Sellasie Avenue pamoja na barabara za Lower na Upper Hill.
Aidha mamlaka ya barabara za mijini nchini KURA kwa upande wake imesema kuwa mbio hizo zitaanzia uwanja wa kitaifa wa Nyayo na kuishia Museum Hill. Hata hivyo barabara ambazo pia zitaathirika ni pamoja na Marathon, Ragati, Hospital Road, Elgon, Matumbato, Masaba, Wakihuri, Bunyala, Commercial, Enterprise, Dar es Salaam, Dunga, Lusaka na Aerodome.
KURA vile vile imewataka wasafiri kutumia njia mbadala jinsi
wataelekezwa na maafisa wa usalama na trafiki.