Tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC inamchunguza meneja katika mamalaka ya bahari nchini kwa madai ya kuhusika na ufisadi wa shilingi 40,539,760 kupitia zabuni.
Maafisa wa EACC kwa waranti ya mahakama, walimkamata Henry Mwasaru mnamo Jumanne Novemba 26, ambaye ni msimamizi wa wafanyakazi na utawala kwenye mamlaka ya KMA, kufuatia madai ya kuhusika katika ufisadi kwenye zabuni ya usamabazaji wa bima ya afya kwa wafanayakazi wa mamlaka hiyo.
Mwasaru alikamatwa katika operesheni ambayo pia ililenga kuwakamata mawakala wawili wa bima wanaoaminika kuwa walishirikiana na meneja huyo kwenye kashfa hiyo ya bima.
Katika madai hayo, Mwasaru anakisiwa kushirikiana na mkuu wa usimamizi wa ugavi kwenye mamlaka hiyo Bevaline Lundu katika kutoa zabuni hiyo ya bima ya afya kwa kampuni moja ya bima kinyume cha sheria.
EACC imesema kwamba tayari imepata ushahidi muhimu ambao utawasaidia wakati wanaendelea na uchunguzi baada ya kuarifiwa mnamo Septemba 30, 2024 kwamba maafisa kadhaa katika mamlaka ya KMA walipeana zabuni kwa kampuni moja kinyume cha sheria.
EACC hata hivyo imesema kwamba inachunguza ununuzi wa bima
ya matibabu ya wafanyakazi katika taasisi za umma ikidaiwa kuwa maafisa wengi
wa serikali hutumia njia hiyo katika ubadhirifu wa fedha za umma.