SERIKALI kupitia wizara
ya leba imetangazia Wakenya wenye ujuzi katika kuendesha bodaboda kuhusu
kupatikana kwa ajira 600 katika jiji la Dubai, kwenye taifa la Miliki za
Kiarabu.
Waziri wa Leba Alfred
Mutua alichapisha tangazo hilo kupitia ukurasa wake wa X, akiwataarifu Wakenya wenye
ujuzi wa kuendesha bodaboda kutuma barua zao za maombi ya kazi.
Waziri Mutua alisema
kwamba mshahara utakuwa shilingi 104,000 ambazo hazitoshwi ushuru.
Mutua alisema kwamba
maafisa kutoka UAE watakuwa nchini Kenya wiki ijayo kutafuta waendesha bodaboda
hao kwa ajili ya kazi hiyo ambayo itakuwa ni ya kupeleka na kurudisha mizigo na
malipo yatakuwa yanahesabika baada ya kila mzunguko mmoja wa safari.
“Maafisa kutoka kampuni
ya Umoja wa Falme za Kiarabu watakuwa nchini Kenya wiki ijayo kuwahoji na
kuwaajiri waendesha pikipiki. Waendeshaji watapata dirham 7.5 kwa kila safari
ya kusafirisha mizigo.”
“Wastani wa chini wa
kila siku ni safari 15, kutafsiri hadi dirham 112.5 kwa siku. Kwa siku 26 za
kazi kwa mwezi, hii ni jumla ya dirham 2,925 (takriban shilingi 104,000 za
Kenya, bila kodi).”
“Wanunuzi walio na
mpango wa kwanza wanaweza kusafirisha bidhaa zaidi ya 30 kwa siku, na kuongeza
mapato yao,” Waziri Mutua alifafanua.
Hata hivyo, waziri Mutua
alieleza kwamba yeyote atakayepata kazi hiyo atahitajika kugharamia ada
mbalimbali zikiwemo usafiri, vipimo vya afya miongoni mwa ada zingine zitakazofika
jumla ya shilingi 167,900 pesa za Kenya.
Lakini pia alifichua
kuwa mpenyo wa yeyote atakayefaulu katika usaili lakini akakosa namna ya kupata
pesa hizo, akisema benki ziko tayari kuwapa mkopo ambao watarejesha baada ya
kuanza kazi Dubai.
“Benki zimeunganishwa
ili kutoa mikopo ili kulipia gharama hizi, kuruhusu wafanyakazi kurejesha pindi
wanapoanza kufanya kazi Dubai. Ada ya matibabu hulipwa kwanza, na gharama
zilizobaki zinaweza kutatuliwa baada ya kupitisha matibabu. Hii inahakikisha
hakuna hasara zisizo za lazima,” Mutua alifafanua kwa
kina.
Usaili utafanyika
Desemba 9-11 jijini Nairobi katika chuo cha kiufundi cha Kamkunji huku Malindi
katika kaunti ya Kilifi usaili ukifanyika Desemba 13-14.