Godfrey Otunge, kamanda wa polisi anayeongoza
opareseni ya maafisa wa polisi kutoka Kenya nchini Haiti amezitaja kama
propaganda za uongo taarifa zinazosambazwa kwamba baadhi ya maafisa wake
wamewasilisha barua za kujiuzulu nchini Haiti.
Hii ni baada ya uvumi kuibuka kwamba karibu maafisa
20 wa polisi wa Kenya nchini Haiti wamewasilisha barua zao za kujiuzulu kwa
serikali kutokana na kucheleweshwa kwa mishahara na mazingira duni ya kazi.
Hata hivyo, Otunge alikanusha taarifa hizo akisema
kwamba vikosi vyake vimejitolea kikamilifu kufanikisha oparesheni hiyo maarufu
kama MSS.
"Wafanyakazi
wote wa MSS wamepokea mishahara yao, ikiwa ni pamoja na posho za kila mwezi, na
hakuna afisa wa MSS aliyewasilisha barua kujiuzulu kama inavyodaiwa,"
alisema katika taarifa.
Alithibitisha kuwa maafisa wa MSS wana ari ya juu na
wamejitolea kikamilifu kusaidia Polisi wa Kitaifa wa Haiti katika kuendesha
operesheni zinazolenga kusambaratisha mitandao ya magenge na kurejesha utulivu.
“Tunawaomba
wadau wote, vikiwemo vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, kutafuta
ufafanuzi moja kwa moja kutoka kwa MSS kabla ya kuchapisha ripoti zozote.
Milango yetu inasalia wazi kwa mawasiliano ya uwazi,”
Otunge alisema.
Shirika la habari la kigeni lilikuwa limeripoti kwamba
karibu maafisa 20 wa polisi wa Kenya nchini Haiti waliwasilisha barua za
kujiuzulu kwa serikali kutokana na kucheleweshwa kwa mishahara na mazingira
mabaya ya kazi.
Habari zilidai kuwa maafisa wanaodaiwa kuwasilisha barua zao
za kujiuzulu walikuwa bado hawajapata majibu kutoka kwa serikali.