Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi amewataka viongozi wa
makanisa kuwa waaminifu kuhusiana na mchango wa pesa kutoka kwa wanasiasa.
Sudi alikashifu baadhi ya makanisa na maaskofu kwa
kukataa michango kutoka kwa Rais William Ruto ilhali amekuwa akiunga mkono makanisa
katika maisha yake yote ya kisiasa.
Mbunge huyo alisema Ruto amekuwa akihudhuria makanisa
na kutoa michango au kutoa zawadi hata alipokuwa mbunge na hivyo basi, haikuwa
vyema kwa baadhi ya makanisa kufanya kana kwamba hakuna mahitaji ndani ya
makanisa.
"Haya
yote yanahusu kazi ya Mungu na hakuna mtu aliye na haki ya kututisha au kusema
hatapokea pesa kutoka kwa Ruto kwa sababu za ajabu,"
Sudi alisema.
“Hata
tumetishwa lakini Mungu huyohuyo alimbariki Ruto kuwa Rais. Yote ni kazi ya
Mungu.”
Mbunge huyo alikuwa akizungumza katika Kanisa la AIC
Pioneer mjini Eldoret ambapo Bibi wa Rais Rachel Ruto pia alihudhuria sherehe
za kuadhimisha miaka 50 ya kuwepo kwa kanisa hilo.
Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii, Mbunge mteule
Joseph Wainaina na Waziri wa Afya Mary Muthoni walikuwa baadhi ya viongozi
wengine waliohudhuria.
Sudi alisema hakuna njia nyingine makanisa au miradi
ya jamii ingejengwa isipokuwa kupitia watu wanaotoa sadaka.
Alisema kwa zaidi ya nusu ya maisha yake, amekuwa
akihudhuria kanisani na kutoa fedha taslimu na hakuna jinsi angezuiwa kufanya
hivyo.
"Nimelelewa
katika familia ya Kikristo na kuhudhuria shule ya Jumapili, ninaamini sana
kanuni ya kibiblia ya kutoa na kuchangia kazi ya Mungu. Ufahamu huu wa maandiko
ndio sababu nitaendelea kutoa kwa kanisa na kusaidia kazi ya Mungu."
"Hata
kama viongozi wakati mwingine tunakuja na kutoa ahadi lakini kwa neema ya
Mungu, kwa kawaida tunapata pesa na kutoa ahadi zetu."
Wainaina pia alipuuzilia mbali wanaokataa michango
akisema hawastahili kuwa viongozi wa kanisa.
Alisema wakati wote huo, Ruto amekuwa mkarimu na wale
wanaokataa michango yake wasifikiri wanamwadhibu.
Mbunge huyo aliwashutumu baadhi ya viongozi wa kanisa
hilo kwa kufanya kazi ya kuwafanya waumini wapoteze imani na Rais.
Sudi wakati huo huo aliwashambulia wanaharakati wa mitandao
ya kijamii ambao wameendeleza ukosoaji dhidi ya miradi na programu za serikali.
Aliwataja kuwa watu "wasiofaa" ambao hawana
la kufanya ila kustawi kwa kuwapotosha Wakenya.
"Niliwaona baadhi yao wakati wa
maandamano ya Gen Z wakipotosha vijana kuchoma nchi hii lakini wao wenyewe
wanaishi nje ya nchi," Sudi alisema.
Mbunge huyo wa Kapseret aliwashutumu watu wa mitandao
ya kijamii kwa kupinga programu bora za serikali kama vile SHA, ambayo alisema
imeundwa kuwezesha Wakenya kupata huduma bora za afya.
"Binafsi
ninahamasisha Wakenya kujisajili na SHA kwa sababu najua itakuwa muhimu hasa
kwa Wakenya maskini," Sudi alisema.
Mbunge huyo na PS Muthoni waliwataka Wakenya
kutoamini wale wanaopinga SHA au kuingiza siasa katika masuala ya afya.