logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Muungano wa matabibu watishia kupiga kambi katika ofisi za wizara ya afya mnamo Jumatano

KMPDU ilitoa ilani ya kuandaa maandamano ya kitaifa kuanzia Disemba 22 mwaka 2024

image
na Brandon Asiema

Habari10 December 2024 - 15:21

Muhtasari


  • Katika kupiga kambi kwake kwenye ofisi za wizara ya afya, KMPDU imesema kwamba watakuwa wanadai haki, heshima na mfumo bora wa afya kwa Wakenya wote.
  • KMPDU, ilitoa notisi ya mgomo wa kitaifa kuanza Disemba 22 ikiwa kufikia wakati huo, mwajiri wake hatakuwa ametimiza makubaliano yaliyoafikiwa.


Muungano wa matabibu na madaktari wa meno nchini KMPDU, umetishia kupiga kambi katika ofisi za wizara ya afya mnamo Jumatano Disemba 15, kulalamikia kutolipwa mishahara ya miezi mitatu kutoka kwa mwajiri wao.

Kupitia ujumbe kwa ukurasa wa X, muungano huo umenyooshea kidole cha lawama kwa mwajiri wake ukimtaka kuwajibikia ahadi zake.

Takribani wiki moja iliyopita, muungano huo ulitoa notisi ya wiki moja kwa serikali kwamba wanachama wake watashiriki mgomo wa kitaifa ikiwa matakwa wanayohitaji kushughuklikiwa na mwajiri wao hayatashughulikiwa kulingana na mikataba baina ya pande zote mbili.

Aidha katika kupiga kambi kwake kwenye ofisi za wizara ya afya, KMPDU imesema kwamba watakuwa wanadai haki, heshima na mfumo bora wa afya kwa Wakenya wote.

Akizungumza katika video kwenye ukurasa wake wa X, katibu mkuu wa KMPDU Davji Bhimji Atellah amemshutumu mwajiri wake kwa kukosa kutekeleza formula ya kurejea kazini iliyoafikiwa mnamo Mei 8, 2024 pamoja na malipo mazuri kwa madaktari wanagenzi.

KMPDU, ilitoa notisi ya mgomo wa kitaifa kuanza Disemba 22 ikiwa kufikia wakati huo, mwajiri wake hatakuwa ametimiza makubaliano yaliyoafikiwa.

“Tulitoa ilani ya maandamano ndani ya siku 21 kwa sababu hatuwezi kuendelea kusimama wakati wafanyakazi wa afya wanazidi kupuuzwa. Mgomo wa kitaifa wa madaktari utaanza Disemba 22, 2024 ikiwa serikali itakosa kutimiza ahadi zake.” Davji Atellah aliandika kwenye ukurasa wake wa X.

Mgomo huo ambao unabakisha siku 12  kung’oa nanga kuanzia Jumanne Disemba 10, unaratibiwa licha ya wizara ya afya mnamo Novemba 30, kutoa shilingi 965,875,345.60 kwa malipo ya madaktari wanagenzi.

Hata hivyo kwenye malalamishi ya KMPDU kupitia katibu wake, imemshtumu mwajiri wake kwa kukiuka maagizo ya mahakama kwamba makubaliano ya CBA kuhusu mishahara ya wanagenzi wa tasnia hiyo lazima ilipwe kwa mujibu wa makubaliano ya CBA ya mwaka 2017.



RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved