SIKU mbili baada ya
kufichua kuwepo kwa mkutano baina yake na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, rais
Ruto amefichua sababu zilizomsukuma kumtafuta nyumbani kwake Ichaweri.
Akizungumza na Jumanne,
Ruto alisema kwamba hatua yake ya kumtafuta rais mstaafu ni kulenga kuzika
tofauti zao katika kaburi la sahau na kuganga yajayo, lengo kuu likiwa ni
kuleta umoja wa taifa kwa kuwahusisha viongozi wote.
Kiongizi wa taifa
alikiri kwamba ni kweli alimtafuta rais mstaafu ili kutafuta mwafaka kuhusu
mustakabali wa nchi.
“Ndio sababu kwamba
ninafanya kazi na waziri mkuu wa zamani, ndio sababu nilimtafuta rais mstaafu,
na ndio sababu nitawatafuta viongozi wote wa kila aina ili kwamba tuweze
kujenga nchi ambayo sisi wote tuna Imani nayo,”
alisema Ruto.
“Ni lazima tuendelee
kujenga madaraja ya kutuunganisha kuliko kujenga kuta za kutugawanya. Ni lazima
muda wote tujenge nguvu ya pamoja tunaposonga mbele,”
Ruto aliongeza.
Hata hivyo, katibu mkuu
wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni alisisitiza kwamba mkutano wa Ruto na Uhuru
haukuwa na lengo la kukijumuisha chama cha Jubilee ndani ya Serikali.
“Hatufanyi mazungumzo na
wewe ili sisi tuingie serikalini, tunafanya mazungumzo kwa sababu ni muhimu kwa
sisi wote kama Wakenya kuzungumza na kila mmoja.”
Hata hivyo, mshauri wa
rais katika masuala ya kiuchumi, Moses Kuria ameonekana kukinzana na Kioni,
akisema kwamba ni muda wa kukifufua chama cha Jubilee huku akitoa maoni kwamba
ni muda wa kurejesha mswada wa BBI.
“Namrai rais William
Ruto na rais mstaafu Uhuru Kenyatta kujadiliana kuhusu uongozi wa nchi na
kufufua BBI, kuipa nchi katiba ambayo itazingatia masuala ibuka ya taifa na
jamii. Awamu ya pili ya BBI inahitajika kwa haraka na haiwezi subiri,”
Kuria alisema.