ALIYEKUWA naibu wa rais,
Rigathi Gachagua amedai kwamba eneo pana la Mlima Kenya sasa alina deni la mtu
yeyote zaidi ya kinara wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka.
Akizungumza katika hafla
moja ya mazishi kaunti ya Makueni, Gachagua alisema kwamba watu kutoka upande
wa Mlima Kenya kazi yao ni ya kulipa madeni ya kisiasa.
Kiongozi uyo alibainisha
kwamba kufikia sasa, wamemaliza kulipa deni la rais William Ruto kwa ujumla na
sasa deni lililosalia ni la Kalonzo Musyoka.
“Sisi tulisahau kulipa
Kalonzo deni lake, liko! Sisi ni watu wa kulipa madeni. Tulikuwa na deni la
Ruto tumemaliza, sisi hatuna deni lake sasa. Tulikuwa tunataka kumlipa kwa awamu
mbili lakini baada ya kumlipa awamu ya kwanza ameleta madharau tumesema hilo
deni limekwisha,” Gachagua alisema.
“Sisi hatyuna deni lake,
tuko huru sasa. Madeni ambayo tunayo ni kidogo kidogo ndio tunataka tulipe ndio
tukae bila deni. Tumebaki tu na Kalonzo na nyinyi,”
Gachagua alisisitiza.
Tamko hilo liliashiria
kwamba huenda Kalonzo akaungana na Gachagua na viongozi wengine katika
kuanzisha mrengo wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Gachagua alithibitisha
kwamba kuna mazungumzo ambayo yanaendelea baina yake na viongozi wengine
akiwemo Kalonzo Musyoka.
Alisema kwamba Kalonzo
alionyesha urafiki wa kweli kusimama naye wakati wa mchakato wa kubanduliwa
kwake ofisini.
“Tunaongea na Kalonzo,
mimi na viongozi wengine kina Eugene Wamalwa na wengine na tutapanga vizuri. Tunafanya
mazungumzo kama Wakenya tukitafuta njia vile tutajipanga vizuri kwa sababu ya
uchumi wa Kenya yetu na tumalize mambo ya uongo katika hii Kenya. Tunataka hii
Kenya isonge mbele,” aliongeza Gachagua.