POLISI wa kitengo cha shirika la reli nchini Tanzania
wamewatia mbaroni zaidi ya watu 13 wakishukiwa kuhusika katika wizi wa vifaa
vya ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR nchini humo.
Kwa mujibu wa kamanda wa kitengo hicho cha polisi,
Hyera Gallus, watu hao walikamatwa wakiwa na vifaa hivyo kinyume cha sheria na
kushtakiwa kwa kosa la uhujumu wa uchumi na wizi wa nyaya za shaba.
Kamanda wa Polisi wa Shirika la Reli, Gallus Hyera,
alionyesha waya zilizoibiwa zilizookotwa katika maeneo mbalimbali.
Alifichua kuwa
washukiwa hao ni pamoja na watu kutoka China, Kenya, na Tanzania, ambao baadhi
yao walikuwa wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi wa reli ya Uturuki, Yapi Merkez.
Kati ya waliokamatwa, wanane walifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha mkoani Pwani, huku watano wakifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam, wote wakikabiliwa na
mashtaka yanayofanana ya uhujumu uchumi.
Kamanda Hyera alieleza kuwa kukamatwa kwa watu hao
kunatokana na operesheni kubwa ya kiintelejensia iliyowezesha polisi kupata
nyaya zilizoibwa na vifaa vingine vya miundombinu ya reli.
Miongoni mwa mshukiwa huyo ni fundi wa umeme
aliyeajiriwa na Yapi Merkez, ambaye kwa mujibu wa polisi alihusika katika
kukata na kuiba nyaya hizo.
Aidha alifichua kuwa wamiliki wa Kampuni ya African
Light Investment inayofanya shughuli zake Visiga Wilaya ya Mlandizi pia
walikamatwa.
Kampuni hiyo inayodaiwa kumilikiwa na watu kutoka
China na Kenya, ilikutwa na waya za shaba zenye uzito wa kilo 882 mali ya
Shirika la Reli Tanzania (TRC).
"Natoa
onyo kwa yeyote anayepanga kuhujumu SGR na miundombinu mingine ya umeme kwamba
hatua kali zitachukuliwa dhidi yao," Kamanda Hyera
alionya.
Aliitaka jamii kuchukua jukumu kubwa katika kulinda
miundombinu ya reli na kutoa taarifa kwa vitendo vya uharibifu au uhalifu.
Mwezi mmoja uliopita, Jeshi la Polisi mkoani Dodoma
liliwakamata watu sita kwa tuhuma za kuharibu na kuiba waya za shaba kwenye
miundombinu ya Reli ya Standard Gauge (SGR) katika wilaya za Mpwapwa na Bahi,
mkoani Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (RPC) George Katabazi
alithibitisha kukamatwa kwa watu hao na kufafanua matukio hayo.