GAVANA wa Vihiga, Wilberforce Ottichilo amevutia
maoni kinzani kutoka kwa Wakenya na wakaazi wa kaunti hiyo ya Magharibi mwa
Kenya baada ya kutangaza kuzindua makafani mapya.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook mnamo Ijumaa Desemba
20, gavana Ottichilo alihudhuria hafla ya kuzinduliwa rasmi kwa mochari hiyo,
akisema ni hatua kubwa katika kueneza huduma kwa watu.
“Hatimaye
iko TAYARI. Kesho TUNAFUNGUA Milango,” sehemu ya
tangazo hilo lilisoma siku mbili zilizopita.
Gavana alitangaza kwamba mochari hiyo imefunguliwa
katika hospitali kuu ya rufaa ya Vihiga ambayo sasa itaongeza huduma kwa
wananchi wanaofariki.
Wakati baadhi walimtetea gavana kwa mochari hiyo mpya
wakisema kifo ni kama ibada kwa kila maisha ya binadamu, wengine walikinzana
naye wakimtaka kuweka kipaumbele kuongeza huduma za matibabu badala ya huduma
za wafu.
Haya hapa ni baadhi ya maoni;
“Wanaomlaani
gavana huyo hawafahamu hali ya chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo Mbale. Kwa
kweli inasikitisha na kuna haja ya hatua za haraka, katika suala hili
nampongeza Wilbur kwa hatua ya kwanza iliyochukuliwa. Ninamsihi aweke hatua za
kutosha kuhakikisha kituo kinakuwa na ufanisi wakati wote,”
Adira Mwigai alisema.
“Kwa
hivyo huwezi kutengeneza barabara, kuweka usalama, kuhakikisha huduma nzuri za
matibabu katika VTRH, kuweka taa za barabarani mijini, lakini kuwa na ujasiri
wa kutufungulia vyumba vya kuhifadhia maiti. Kwa ajili ya mbinguni Wilber
Khasilwa Ottichilo unataka tuwe hai au tuwe hai,”
Denis Avoga alisema.
“Wakati
Wamatangi mjini Kiambu inaboresha hospitali na vituo vya ECDE, Gavana wetu
anawekeza katika nyumba za mazishi.” Martin Ikojeri.
“Hii
ilipaswa kufunuliwa kimyakimya (Chini ya Maji). Kaburi, jeneza na chumba cha
kuhifadhi maiti havijawahi kuwa alama za sherehe huko Luhyaland. Mkazo unapaswa
kuwa katika kuendeleza vituo vinavyoboresha afya bora na maisha bora kwa watu
wetu.” Naviava Wilson.
“Badala
ya kuwekeza katika hospitali ya rufaa ya Vihiga ili kuboresha huduma zake
unaweka pesa katika kujenga chumba cha kuhifadhia maiti”
Jackson Okata.
Maoni yako ni yepi?